Aliyekuwa Katibu wa Watia Nia wa Ubunge kupitia kundi maarufu la G55, Edward Kinabo, ametangaza rasmi kujiondoa katika chama hicho. Akiwahutubia waandishi wa habari, Kinabo alisema kuwa hali ndani ya CHADEMA ni mbaya zaidi kuliko changamoto zinazotoka nje ya chama.
“Ndani ya chama chetu hali si shwari. Wahenga walisema, mficha maradhi kifo humuumbua. CHADEMA si chama kile tena tulichokijenga. Kimepoteza mwelekeo na sasa kinatoka kabisa kwenye mstari wa vyama vya siasa vyenye msingi wa kidemokrasia,” alisema Kinabo.
Akiendelea kufafanua, Kinabo alibainisha kuwa hatua yake haimaanishi kuacha siasa, bali ni kutafuta njia mbadala ya kuendeleza falsafa ya mabadiliko kupitia vyama vingine.
“CHADEMA sasa kina makundi mawili ndani ya chama kimoja. Uongozi umeshindwa kukiunganisha chama na wanachama. Huu siyo mwelekeo tuliotarajia,” alisema.
Kinabo, ambaye amekuwa mwanachama wa CHADEMA kwa zaidi ya miaka 20, alieleza kuwa amekuwa akijaribu kulisaidia chama kwa ushauri, lakini juhudi hizo zimekuwa zikipuuzwa.
“Mpango wa chama kujaribu kuzuia uchaguzi ni hatari kwa taifa. Badala ya kushiriki na kushinda kwa hoja, wanatoa wito wa kususia uchaguzi. Hii siyo demokrasia, na tukisema ukweli tunaonekana wasaliti.”
Aliendelea kueleza masikitiko yake kuhusu namna mwenyekiti wa chama, Freeman Mbowe, anavyodhalilishwa ndani ya chama:
“Mbowe anadhalilishwa na baadhi ya wanachama. Wanaomuunga mkono wanaonekana kama waasi. Huu si uongozi wa maono bali wa visasi.”
Mbali na Kinabo, Eliya Evalist, aliyekuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu Wilaya ya Temeke, pia alitangaza kujiondoa CHADEMA kwa sababu ya kile alichokiita chuki na mgawanyiko usiomalizika.
“Wanasema tumenunuliwa, lakini Heche si tofauti na madalali wengine. Gari analotumia kadi yake inasomeka kwa jina la mke wa Waziri mmoja kutoka CCM. Hii ni aibu kwa chama kinachojinasibu kuwa cha mabadiliko,” alisema Evalist.
Naye Salma Sharifu, aliyekuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu kupitia Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA) Taifa, aliondoka kwa hisia akieleza mateso aliyopitia kwa kuwa upande wa Mbowe.
“Nilinyanyaswa na kubaguliwa kwa kuwa upande wa Mbowe. Nimepoteza ndugu zangu kwa sababu ya CHADEMA. Huu siyo upinzani wa kweli tena. Naamini muda umefika wa kuendelea na harakati mahali pengine,” alisema Salma kwa maumivu.
Viongozi hao watatu wametoa wito kwa wanachama wengine waliokata tamaa ndani ya CHADEMA kuungana nao katika kuendeleza harakati za kisiasa nje ya chama hicho, wakisisitiza kuwa mabadiliko ya kweli hayawezi kupatikana katika mazingira ya migawanyiko na ubaguzi wa ndani.

0 Comments:
Post a Comment