Viongozi wa Dini Watoa Wito wa Haki na Maridhiano: “Waachiwe Bila Masharti Waliokamatwa Kwa Kudai Haki



Katika kipindi hiki muhimu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, viongozi wa dini nchini Tanzania wameungana kwa sauti moja wakisisitiza umuhimu wa haki, maridhiano na amani ya kweli. Wametumia madhabahu ya Pasaka kutoa kauli zenye uzito mkubwa kwa Serikali na vyombo vyake, wakitaka hatua za dhati zichukuliwe kuhakikisha siasa za nchi zinaendeshwa kwa misingi ya haki, uhuru na maridhiano.

TEC: Viongozi wa Kisiasa Waliokamatwa Waachiwe Bila Masharti




Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), kupitia kwa Rais wake ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki Lindi, Mhashamu Wolfgang Pisa, limetoa wito kwa Serikali kuwaachilia mara moja na bila masharti viongozi wa kisiasa waliokamatwa kwa kudai haki.

“Amani ya kweli haiwezi kupatikana kwa kutumia nguvu bali kwa maridhiano na haki,” amesema Askofu Pisa, akiongeza kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda amani kwa kuhakikisha mifumo ya uchaguzi inarekebishwa ili kutoa nafasi kwa upatikanaji wa viongozi wa haki na wa kweli.

Akizungumza katika mkesha wa Pasaka katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Andrea Kagwa, Lindi, Askofu Pisa alihoji:
“Katika hali ya kawaida, nani anaharibu amani? Anayetumia nguvu na kusisitiza uchaguzi uende anavyotaka yeye au yule anayesema ‘jamani turudi mezani ili tuangalie mifumo yetu ya uchaguzi kwani mifumo ya sasa haiwezi kutupatia viongozi wa haki na kweli’?”

Aliendelea kusisitiza:
“Kwa maana hiyo wote waliokamatwa kwa kudai haki, wakiwemo viongozi wa vyama vya kisiasa, waachiwe haraka na bila masharti, na wengine wasikamatwe wala kusumbuliwa. Pia mihimili isiingiliwe bali itende kazi zake kwa haki.”

DCT: Serikali na CHADEMA Wakutane Meza ya Mazungumzo

Askofu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT), Dkt. Dickson Chilongani naye amesisitiza kuwa suluhu ya kweli ya mvutano wa kisiasa ni mazungumzo ya pande husika.

“Tumesikia juzi pamoja na nchi yetu kuwa haina vita, lakini watu wake hawana furaha... Tungeomba viongozi wa pande zote mbili wakae pamoja wamalize tofauti zao kwa njia ya mazungumzo,” alisema Askofu Chilongani kwenye Ibada ya Pasaka katika Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu, Dodoma.

Aliitaka Serikali kutatua kero kama rushwa, ubadhirifu na ukiritimba ambazo zinakwamisha ustawi wa taifa.

KKKT: Amani Isibebwe na Kauli Bali Matendo ya Haki

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dkt. Alex Malasusa, alihimiza watanzania na wanasiasa kuendeleza utamaduni wa kutunza amani.
“Tuna wajibu wa kulinda amani. Hebu tuwe wapatanishi. Ikiwa utakosa kitu cha kujenga cha kusema, ni bora kukaa kimya kuliko kuzungumza maneno ambayo yanaweza kuchochea migogoro,” alisema kwenye Ibada ya Pasaka Parokia ya Azania Front, Dar es Salaam.

Aidha, aliwataka wanasiasa wanaotarajia kugombea nafasi mbalimbali kufika kanisani kwa ajili ya maombi.
“Wanaotarajia kugombea nafasi hiyo wanakaribishwa kufika kanisani kwa maombi, tutakuombea ili Mungu akuongoze katika safari hii,” aliongeza.

Askofu Shoo: Vyombo vya Dola Viheshimu Maamuzi ya Wananchi

Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT, Askofu Dkt. Fredrick Shoo, ametoa wito kwa vyombo vya dola, hasa Jeshi la Polisi, kuhakikisha havitumiki vibaya wakati wa uchaguzi.

“Ni wakati wa Tanzania kuandika historia mpya ya uchaguzi wa kidemokrasia unaozingatia amani, usawa na maridhiano ya kweli,” alisisitiza katika ibada ya Pasaka mjini Moshi.

Askofu Mwaikali: Tuombee Taifa, Tuchague Viongozi Wenye Hofu ya Mungu

Askofu wa Kilutheri Nyanda za Juu Kusini, Dkt. Edward Mwaikali, naye ameongeza sauti yake katika kutetea amani.
“Amani ya nchi yetu ikitoweka hatutapata mbadala wa nchi nyingine... Hii amani iliyopo, viongozi wa Serikali wamejitahidi sana, lakini siyo peke yao. Watumishi wa Mungu wa dini zote wamehusika,” alisema katika ibada ya Pasaka, Ruanda.

Aliwahimiza waumini kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
“Itapendeza sana kuona kiongozi akiwa mtumishi wa Mungu kwa kuwa hofu itakuwapo kuliko kuwaachia wengine,” alisema, akibainisha kuwa tayari kuna muumini mmoja kanisani kwake ambaye amejitokeza na ameanza kuombewa.

Rais Samia: Pasaka Iwe Tafakari ya Upendo, Haki na Uadilifu



Kupitia salamu zake za Pasaka, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa wito wa kitaifa wa mshikamano na amani.



“Siku hii njema ikawe pia ya tafakari kwetu sote juu ya upendo wetu kwa Muumba wetu na wenzetu; juu ya kujitoa kwa bidii na weledi katika utekelezaji wa majukumu yetu... juu ya haki ambazo daima huambatana na wajibu,” ameandika Rais Samia.



Kauli hizi kutoka kwa viongozi wa dini zinaakisi uhitaji wa haraka wa maridhiano ya kitaifa, mazungumzo ya kisiasa, na utekelezaji wa haki katika mchakato mzima wa uchaguzi. 


Kwa sauti moja, viongozi hawa wameweka mbele maslahi ya taifa, wakisisitiza kuwa amani ya kweli haiwezi kufanikishwa pasipo haki na usawa. Ni wakati wa kuisikiliza miito hii na kuchukua hatua stahiki kwa ajili ya mustakabali wa Tanzania.

0 Comments:

Post a Comment