TANAPA Yasisitiza Kubuni Mazao Mapya ya Utalii kwa Kushirikiana na Jamii Inayozunguka Hifadhi ya Taifa Milima ya Udzungwa

 


“Niwapongeze kwa elimu mnayoitoa kwa jamii kuhusu uhifadhi na utalii, tunaenda vizuri nisisitize kubuni mazao mapya ya utalii kwa kushirikiana na jamii inayozunguka hifadhi.” 



Haya ni maneno ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Jenerali (Mstaafu) George Waitara, aliyoitoa wakati wa ukaguzi wa miradi inayotekelezwa na Mradi wa REGROW katika Hifadhi ya Taifa Milima ya Udzungwa, mkoani Morogoro, Aprili 8, 2025.



Katika hatua hii, TANAPA imeagiza Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Milima ya Udzungwa kubuni mazao mapya ya utalii ambayo yatahusisha na jamii inayozunguka hifadhi hiyo, ili kuongeza mapato na kuboresha uhifadhi wa mazingira.

Jenerali Waitara aliwashukuru wahusika kwa kutoa elimu kuhusu uhifadhi na utalii, akisisitiza kuwa ni muhimu jamii zinazozunguka hifadhi zichangie zaidi katika kukuza utalii na kuhakikisha uhifadhi wa rasilimali za taifa. 


“Tunaenda vizuri na nisisitize kubuni mazao mapya ya utalii kwa kushirikiana na jamii,” alisema.

Dkt. Robert Fyumagwa, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini TANAPA, aliongeza kuwa ni muhimu kuendelea kuwekeza katika elimu ya uhifadhi na utalii kwa jamii inayozunguka hifadhi. 


Alipongeza juhudi za Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Milima ya Udzungwa katika kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa utalii na uhifadhi.



Kwa upande mwingine, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara TANAPA, Massana Mwishawa, alisisitiza mafanikio ya Shirika katika kuhifadhi misitu na wanyama wa aina mbalimbali katika hifadhi ya Milima ya Udzungwa. 


“TANAPA kupitia Hifadhi ya Taifa Milima ya Udzungwa imeshuhudia ongezeko kubwa la watalii na mapato, lakini lengo kuu la kuanzishwa kwa hifadhi hii ni kulinda bioanuai na vyanzo vya maji, na hili tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa,” alisema Mwishawa.



Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Dora Batiho, ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Milima ya Udzungwa, alieleza kuwa miradi ya REGROW inatekelezwa kwa ufanisi na imeleta manufaa kwa jamii zinazozunguka hifadhi hiyo. 



Alisema kuwa, “Hifadhi inatekeleza Mradi wa Ujenzi wa miundombinu ya utalii (Canopy Walkway), na jamii zinazozunguka hifadhi zimenufaika kupitia Benki Hifadhi za Jamii ‘Community Conservation Bank’ (COCOBA). 

Jumla ya shilingi milioni 568 ilitolewa kwa vikundi 35 katika vijiji vya Mang'ula B, Msufini, na Msosa, vikundi vya wanachama 590.”



Vikundi hivi vimeweza kuanzisha miradi mbalimbali ya kilimo, ufugaji, na biashara ndogondogo, na kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya jamii. 

Miradi hiyo inajumuisha kilimo cha mpunga, miwa, na nyanya, ufugaji wa kuku wa mayai, kuku wa nyama, bata, samaki, na nyuki, pamoja na biashara za mapambo, mashine za kusaga, na kukoboa nafaka.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Msufini, Bw. Nicodem Mwalongo, alieleza faida kubwa zinazopatikana kupitia miradi ya REGROW na COCOBA. 

Alisema, “Faida za miradi hii ni pamoja na kuboreka kwa hali ya uhifadhi wa mazingira, kuimarika kwa mahusiano kati ya hifadhi na jamii, kuboresha makazi ya wanachama, kuanzisha biashara ndogondogo na maduka, na kuongeza mashamba kwa kutumia kilimo cha kisasa. Vilevile, mradi huu umeleta manufaa kwa watoto 54 kwa kutoa elimu bora na pia wanachama wamepata uhakika wa bima ya afya.”

Kwa ujumla, juhudi hizi za ushirikiano kati ya TANAPA na jamii zinazozunguka Hifadhi ya Taifa Milima ya Udzungwa zinasaidia kuongeza thamani ya utalii, kuboresha uhifadhi wa mazingira, na kuleta maendeleo endelevu kwa jamii. 

Miradi kama hii ni mfano mzuri wa jinsi ushirikiano wa karibu kati ya hifadhi na jamii unaweza kuleta mafanikio kwa pande zote.


Source; TANAPA 

0 Comments:

Post a Comment