Mchome Amtaka Lissu Akubali Kukosolewa, Ajiapiza kuilinda Chadema

 


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinazidi kushuhudia mvutano wa ndani, ambapo Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mwanga, Lembrus Mchome, ameibuka kusema  wanaopinga kushiriki uchaguzi watahatarisha uhai wa chama na kuwaathiri wanachama.

Aidha Mchome, amekosoa vikali msimamo wa viongozi wa chama wanaotaka kususia uchaguzi. 

Alisema kuwa misimamo hii ni kinyume na haki za wanachama na inaweza kupelekea chama kupoteza mwelekeo katika siasa za nchi.

"Nilimuandikia barua rasmi kumweleza maoni yangu, lakini majibu yake yalikuwa ya kunizodoa. Hii siyo afya kwa chama kinachodai kuheshimu katiba na demokrasia ya kweli," alisema Mchome, akielezea masikitiko yake kuhusu jinsi maoni yake yalivyokubalika kwa dhihaka badala ya kutafakariwa kwa uzito unaostahili.

Aidha, Mchome alisisitiza kuwa chama kinapaswa kuzingatia sheria za vyama vya siasa, na kwamba Msajili wa Vyama anapaswa kuwa mlezi wa utekelezaji wa katiba na miongozo ya vyama. 


Alitoa wito kwa viongozi wa chama hicho kufuata taratibu na kuzuia matumizi mabaya ya mamlaka kwa kudhibiti mijadala ya msingi ndani ya chama.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 8, 2025 jijini Dar es Salaam, Mchome alisisitiza kuwa ni muhimu kwa CHADEMA kuwa chama cha mfano katika kushiriki kikamilifu katika michakato ya uchaguzi. 


Aliamini kuwa kujitenga na uchaguzi kutaleta madhara makubwa kwa chama hicho.

"Watanzania watambue nitafanya haya kwa ajili ya kukilinda chama changu kesho na keshokutwa. Hoja zangu zina mashiko na lengo ni kukisaidia chama, si kukivuruga," alisisitiza Mchome.

Pia, alieleza mshangao wake kuhusu baadhi ya viongozi wa chama wanaojiita wafuasi wa demokrasia lakini wanaendelea na misimamo ya kuzuia kushiriki uchaguzi. 


Alihoji kuwa hatua hiyo ni sawa na kuua chama kwa makusudi.

"Leo tuna kiongozi mkuu wa chama hataki kukosolewa. Aliwahi kumuita hayati Rais Magufuli dikteta, lakini sasa hali inayojitokeza ndani ya chama si tofauti na hiyo. Hatupaswi kuwa na hofu ya hoja mbadala," aliongeza.

Mchome hakusita kuzungumzia changamoto aliyonayo na mwenyekiti wa chama, Tundu Lissu. 


Alimshauri Lissu kuwa miongoni mwa majukumu yake kama kiongozi mkuu wa chama ni kuwa wazi kwa kukosolewa na kupokea maoni ya wanachama, badala ya kutumia matusi kwa wale wanaopinga baadhi ya maamuzi ya chama.

"Hutaki kukosolewa umekuwa Mungu, kwanini tusikukosoe, tusikuseme na tusilete hoja mbadala ambazo wewe kama Mwenyekiti wa Chama Taifa unapaswa kukaa chini kuziangalia kama unaweza kuzipokea au kuzipuuza?" alisisitiza Mchome.

“Nimuombe Mwenyekiti wangu akubali kukosolewa ili tuijenge Chadema imara, taasisi yenye nguvu na kukuza umoja wetu tuliokuwa nao hapo awali, wala hana haja ya kututukana,” aliongeza Mchome.

Akizungumzia msimamo wa baadhi ya viongozi wa chama kutaka kususia uchaguzi, Mchome alisema kuwa anaamini kuwa CHADEMA kisiposhiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, kitajiingiza katika shida kubwa na pengine kupoteza imani ya Watanzania.

“Mimi ninaamini kwamba CHADEMA tusipoenda kwenye uchaguzi, tutakiua na kukimaliza chama hiki pia tutakichimbia kwenye kaburi hatutaweza kutoka tena, chama hiki tumekijenga kwa jasho kubwa sana na wengine tumekuwa wahanga wakubwa, mimi tangu mwaka 2007 nikiwa kijana mdogo nilijiunga nimetoa rasilimali zangu na kutumia mali zangu nyingi, hivyo hatuwezi kukubali kuona chama hiki kinakwenda kaburini,” alisema Mchome kwa huzuni.

Alisisitiza kuwa chama kilijengwa kwa juhudi kubwa na kuhoji kama kuna faida yoyote kwa viongozi wanaosema kuwa wanatumika ili kumkinga Rais Samia Suluhu Hassan asipate upinzani mwaka huu.

“Leo mwenyekiti unasema wale ambao wanataka kushiriki katika uchaguzi wanatumika tuambie wanatumika na nani na kwa faida gani, na sisi tukisema wale ambao hawataki tushiriki uchaguzi mkuu ndio wanaotumika ili Rais Samia asipate upinzani mwaka huu tutakosea,” alihoji Mchome.

Mchome aliweka wazi kuwa lengo lake ni kuhakikisha chama kinajikita katika misingi ya demokrasia na haki, na kwamba hakubali kuona CHADEMA ikiteketea kwa sababu ya maamuzi yasiyofaa.

0 Comments:

Post a Comment