Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu, leo Aprili 22, 2025, amechukua rasmi fomu ya kuomba kuteuliwa kuwa mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Zoezi hilo limefanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya ACT Wazalendo zilizopo Dar es Salaam, ambapo fomu hiyo alikabidhiwa na Katibu wa Oganaizesheni, Mafunzo na Uchaguzi wa chama, Shaweji Mketo.
Akizungumza mara baada ya kupokea fomu, Dorothy Semu alisema hatua hiyo inaashiria dhamira yake ya kweli na utayari wa kuingia katika kinyang’anyiro cha kuwania urais kwa lengo la kuleta mabadiliko ya msingi nchini.
“Nimechukua fomu hii kama ishara ya utayari wangu wa kumkabili Rais Samia Suluhu Hassan na Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa sababu wameshindwa kuendesha nchi na kuwakomboa Watanzania kiuchumi, kisiasa na kijamii,” alisema Semu.
Aliongeza kuwa hatua hiyo pia ni sehemu ya jitihada zake za kusimamia haki za raia na kuimarisha misingi ya kidemokrasia nchini.
“Nimechukua fomu kama ishara ya utayari wangu wa kuongoza mapambano ya kulinda thamani ya kura na misingi ya demokrasia nchini,” alisisitiza.
Dorothy Semu alieleza kuwa atazungumza na taifa kueleza dira na maono yake kuhusu uongozi wa nchi siku ya kurudisha fomu hiyo, tarehe ambayo ataitangaza hivi karibuni.
“Nitatoa hotuba kwa taifa kueleza dira na maono yangu siku nitakayorudisha fomu, na tarehe hiyo nitaitangaza muda si mrefu,” alisema.
Hatua hiyo inaweka msingi wa mchuano mkali wa kisiasa ndani ya ACT Wazalendo na pia kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kuvutia ushindani mkubwa kati ya vyama vikuu nchini.

0 Comments:
Post a Comment