Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche, amekamatwa na Jeshi la Polisi leo katika eneo la Mkunguni, Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Heche alikamatwa muda mfupi baada ya Polisi Wilaya ya Kariakoo kuwasilisha barua kwa chama hicho, wakizuia mkutano wa hadhara uliokuwa umepangwa kufanyika katika mtaa wa Nyamwezi na Mkunguni.
Barua hiyo ya Polisi ilieleza kuwa mkutano huo haukuruhusiwa kutokana na shughuli nyingi za biashara zinazoendelea katika eneo hilo, ambazo zingetatizwa na mkusanyiko wa watu.
Chadema ilikuwa imepanga kufanya mkutano huo kama sehemu ya kampeni za kutoa elimu kwa umma kuhusu mchakato wa uchaguzi na hali ya kisiasa nchini, lakini jeshi la polisi lilisimamia kusitishwa kwake.
Hadi sasa, haijafahamika ni wapi alipopelekwa Heche na Jeshi la Polisi bado halijatoa taarifa rasmi juu ya sababu za kumkamata. Wafuasi na viongozi wa Chadema wameeleza kusikitishwa na hatua hiyo, wakisema inalenga kuvuruga harakati zao za kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.

0 Comments:
Post a Comment