CHADEMA, chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, sasa kinajikuta kikiwa kwenye njia panda huku makundi mawili yakipingana kuhusu msimamo wa chama juu ya uchaguzi mkuu wa 2025.
Upande mmoja unasisitiza msimamo wa "No Reforms, No Election" (hakuna uchaguzi bila mabadiliko ya sheria), na upande mwingine ukiona umuhimu wa kushiriki uchaguzi bila ya marekebisho ya sheria.
Kila upande hoja zenye nguvu, lakini pia kila uamuzi unakuja na gharama yake.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA Students Organisation - CHASO), Leonce Martin, amekosoa vikali kundi la G55, akilieleza kuwa kundi hilo ni waasi ndani ya chama.
Martin alisisitiza kuwa wanachama wa G55 wanatamani kugombea ubunge kwa maslahi yao binafsi, na kwa kuwa CHADEMA imesisitiza kutoshiriki uchaguzi bila mabadiliko ya sheria za uchaguzi, kundi hilo limeamua kutoafikiana na msimamo wa chama.
“Watu hawa wanatamani kugombea ubunge katika majimbo mbalimbali, na kwa kuwa CHADEMA imesisitiza kutoshiriki uchaguzi bila marekebisho ya sheria za uchaguzi, wameamua kwenda kinyume na msimamo huo kwa maslahi yao binafsi,” alisema Martin akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa CHASO kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Martin Kambore, aliongeza kuwa bila marekebisho ya sheria ya uchaguzi, ni vigumu kupata uchaguzi wa haki na huru nchini.
Kambore alisema kuwa sera ya CHADEMA ya "No Reform, No Election" ni muhimu kwa sababu sheria zilizopo sasa zinawapa fursa walio na uwezo wa kifedha kushinda chaguzi badala ya kushinda kwa misingi ya sera na uadilifu.
“Bila Tume Huru ya Uchaguzi, taifa litaendelea kupata viongozi wasiowajibika kwa wananchi, ambao hawawezi hata kukosolewa wanaposhindwa kutekeleza majukumu yao,” alisisitiza Kambore.
Migawanyiko Ndani ya CHADEMA: G55 na Msimamo wa "No Reform, No Election"
Msimamo wa CHASO unakuja katika kipindi ambacho mjadala kuhusu umuhimu wa marekebisho ya sheria za uchaguzi unaendelea kushika kasi nchini.
Ingawa CHADEMA imekuwa na msimamo wa kutoshiriki uchaguzi bila mabadiliko ya sheria, baadhi ya makundi ndani ya chama, ikiwa ni pamoja na kundi la G55, wameonekana kutofautiana na uongozi wa chama.
Kundi la G55 linaundwa na wanachama ambao wanatofautiana na msimamo wa chama kuhusu "No Reform, No Election".
Hawa wanashinikiza chama kuzingatia maslahi ya Chama na wanachama, na kwa upande mwingine, wanatoa wito kwa chama kushiriki uchaguzi huku wakiendelea na mapambano ya kudai mabadiliko ya sheria.
Hii inafanya mzozo huo kuwa vigumu kusuluhisha kwa urahisi.
Wito wa Majadiliano: Kurejesha Umoja Ndani ya CHADEMA
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa, ametoa wito kwa uongozi wa CHADEMA kuketi meza moja na kundi la G55 ili kumaliza mzozo huu kwa njia ya mazungumzo.
Alisema kuwa kutafuta suluhu ya pamoja kati ya pande hizi mbili ni muhimu kwa kudumisha mshikamano ndani ya chama.
"Rafiki zangu Lissu, Heche, Lema na Mnyika tafuteni namna mkae na G55 yenu. Tupo tayari kusaidia majadiliano haya kati ya uongozi wa chama na G55 ili tuendeleze utamaduni wa mazungumzo pale tunapotofautiana kimitazamo," alisema Ole Ngurumwa kupitia ukurasa wake wa X (Twitter).
Kilio cha Uongozi wa CHADEMA: Kuweka Umoja Kwenye Kipaumbele
Kwa sasa, uongozi wa CHADEMA unapaswa kutumia busara ya hali ya juu ili kuzuia chama kutengeneza nyufa kubwa.
Ikiwa wataendelea kupuuza hoja za G55, kuna hatari ya kukosea kisiasa, ingawa watazikubali na kuzijadili, watatoka wakiwa wamoja iwe wamekubaliana au wametofautiana.
Kama ilivyokuwa kwa vyama kama CUF na NCCR-Mageuzi, ambayo vilikumbwa na mizozo ya ndani na hatimaye kupoteza nguvu zao kisiasa, CHADEMA inapaswa kuchukua tahadhari ili kuepuka mkwamo unaoweza kuathiri umoja na ushawishi wa chama.
CHADEMA inakutana na changamoto kubwa ya kuepusha migawanyiko ya ndani, hususan mzozo kati ya kundi la G55 na uongozi wa chama kuhusu msimamo wa "No Reform, No Election". Uongozi wa chama unahitaji kutumia busara kubwa ili kuhakikisha chama kinasonga mbele kwa umoja na mshikamano, huku wakihakikisha kuwa msimamo wao kuhusu mabadiliko ya sheria za uchaguzi unalinda maslahi ya wananchi.
Vinginevyo, CHADEMA kinaweza kuingia katika mzozo mkubwa na kupoteza nafasi yake muhimu katika siasa za Tanzania.



0 Comments:
Post a Comment