Jaji Mutungi: Kauli ya “No Reform, No Election” si Kosa la Kisheria, Uchaguzi Mkuu 2025 Utafanyika Kama Ilivyopangwa




Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania, Jaji Francis Mutungi, amesema kuwa kauli ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ya kusema “No reform, no election” haivunji sheria yoyote ya vyama vya siasa, na hivyo haitazuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma baada ya kushiriki warsha ya wadau wa uchaguzi kuhusu namna ya kuzuia na kupambana na rushwa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025, Jaji Mutungi alisisitiza kuwa uchaguzi huo utafanyika kama kawaida na hakuna chama au mtu binafsi mwenye mamlaka ya kuuzuia kwa maneno ya majukwaani.

“Hakuna mtu anayeweza kuzuia uchaguzi kwa kutamka tu kwenye jukwaa. CHADEMA hawajavunja sheria yoyote. Nilipokutana nao hivi karibuni walisema hawako tayari kuvunja sheria za uchaguzi,” alisema.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi wa ndani ya chama hicho, CHADEMA wamekuwa wakisisitiza kuwa bila kufanyika kwa mabadiliko ya msingi katika mfumo wa uchaguzi, hawatashiriki uchaguzi mkuu wa 2025, na wametangaza kuwa wako tayari kuandamana nchi nzima kupinga uchaguzi huo. Kauli hiyo imeibua mjadala mkali miongoni mwa vyama vingine vya siasa, wakiwemo CCM, ambacho kimepinga vikali msimamo huo.

Msajili Mutungi amefafanua kuwa chombo pekee chenye mamlaka ya kuzuia uchaguzi ni mahakama, na mpaka sasa hakuna chama kilichofungua kesi kuhusu suala hilo. Ameeleza kuwa kinachoendelea ni matamshi ya kisiasa ambayo hayawezi kuchukuliwa kama uhalisia wa kisheria.

“Kwa sasa, kinachosemwa ni maneno ya kisiasa. Hajasikika mtu au chama chochote kikipeleka shauri hilo mahakamani. Na kama ambavyo sheria inavyosema, mahakama pekee ndiyo yenye mamlaka ya kutoa uamuzi wa kuzuia au kuahirisha uchaguzi,” aliongeza.

Aidha, amesema Ofisi yake itaendelea kusikiliza maoni na malalamiko ya vyama vyote vya siasa kwa haki na usawa, lakini akasisitiza kuwa hakuna chama kinachoruhusiwa kuvunja sheria kwa kisingizio cha kudai mabadiliko.

“Mimi nitatafuta muda wa kuwaita viongozi wa CHADEMA tuzungumze kwa kina kuhusu jambo hili. Kama msajili, nina wajibu wa kuhakikisha kila chama kinashiriki katika mchakato wa kisiasa kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Jaji Mutungi amehitimisha kwa kusema kuwa taasisi yake haitafumbia macho vitendo vya uvunjifu wa sheria kuelekea uchaguzi mkuu, huku akitoa wito kwa vyama vyote kushiriki katika mchakato huo kwa njia ya kidemokrasia na kwa kufuata misingi ya sheria.

0 Comments:

Post a Comment