CHADEMA: Waliamsha Dude Kufanya Mikutano Siku 47; Wamuonya Wasira Asijipe Usemaji wa Mambo yao


Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeibua mjadala mkubwa kuhusu uchaguzi wa mwaka huu na kauli mbiu yake ya "No reform, no election" (Bila mabadiliko, hakuna uchaguzi). 



Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo, MChi 19, 2025 Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Amani Golugwa, alieleza kushtushwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwemo Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, kugeuka kuwa wasemaji wa msimamo wa chama hicho.


Golugwa alisema: “Watu wa CCM, siku hizi wamegeuka kuwa wasemaji wetu, sisi tuna msemaji wetu mmoja tu, lakini ukiwasikiliza Wasira, amekuwa kama msemaji wetu. Ukimsikiliza Makala (Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM), amekuwa kama msemaji wetu, wanatusaidia kufikisha ujumbe lakini sasa wanaharibu kitu ambacho wala hawaelewi.”


Golugwa alisisitiza kuwa kauli mbiu ya "No reform, no election" inasema kuwa uchaguzi hauwezi kufanyika bila kufanya mabadiliko ya kimsingi katika mfumo wa uchaguzi. Aliendelea kusema: “Sisi tunajua namna ya kuielezea hii kaulimbiu yetu, Kiswahili chake kinasema bila mabadiliko hakuna uchaguzi, sasa mzee Wasira wewe siyo msemaji wetu, acha kutusemea kitu ambacho hukielewi, tutakuelewesha mabadiliko yanayotakiwa.”

Aliongeza kuwa, “Kwa hiyo mimi naamini baada ya wiki mbili za ziara kule Nyasa ataelewa Kiswahili chake ambacho anasema haelewi."

Kauli hiyo inakuja ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya ziara ya chama hicho, ambayo itaanza rasmi katika kipindi cha siku 47, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuelimisha wananchi kuhusu msimamo wao kuhusu uchaguzi. Ziara hiyo inatarajiwa kumalizika Mei mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi, kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Golugwa alisema: "Na sisi CHADEMA, hatuweki mpira kwapani, hatukimbii, uchaguzi tutashiriki, lakini tutashiriki tukiwa tumekubaliana mabadiliko yamefanyika."

Kwa mujibu wa Golugwa, kauli mbiu ya ziara ya chama hicho kwa awamu ya kwanza inasema ‘Bira ya mabadiliko hakuna uchaguzi’.


Lengo la ziara hiyo ni kuelimisha wananchi juu ya msimamo wa chama kuhusu mabadiliko muhimu ambayo yanahitajika kabla ya uchaguzi mkuu.

Aidha, Golugwa alitangaza kuwa ziara hii itakuwa na lengo la kupokea wanachama wapya, ikiwa ni sehemu ya kurudisha imani ya wananchi kwa chama hicho, na kueleza kuwa viongozi wa chama hicho hawatakubali kushiriki uchaguzi bila kuwepo kwa mabadiliko ya kimsingi katika mfumo wa uchaguzi wa nchi.

Ziara hii itakuwa ni hatua muhimu kwa CHADEMA, hasa ikizingatiwa kuwa imekuwa na mpito wa uongozi mpya ukiongozwa na Mwenyekiti wake, Tundu Lissu, ambaye alichaguliwa hivi karibuni. Hii ni mara ya kwanza kwa CHADEMA kuanzisha ziara hii baada ya uchaguzi wa uongozi mpya.

0 Comments:

Post a Comment