Biteko Awaasa Wananchi Monduli Kutogawanywa kwa Dini Wala Siasa, Azindua Mradi wa Maji Esilalei

 


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, amewaasa wananchi wa Monduli kutogawanyika kwa misingi ya dini, siasa wala ukabila, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, akisisitiza mshikamano kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.


Akizungumza Aprili 23, 2025 katika Kijiji cha Esilalei, Wilaya ya Monduli mkoani Arusha, mara baada ya kuzindua mradi wa maji katika kijiji hicho, Dkt. Biteko amesema:
“Ninatamani kuona hatugawanyiki na mtu yoyote wala hatuwekwi kwenye makundi ya dini wala ukabila. Nataka niwaombe wananchi wa Monduli pendaneni na shirikianeni, na uchaguzi utakapofika chaguaneni kwa haki.”

Akizungumza kuhusu mradi huo wa maji, aliwapongeza wananchi na Wizara ya Maji pamoja na RUWASA kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa mradi huo:
“Nawapongeza Wizara ya Maji na RUWASA kwa kusimamia mradi huu mzuri na wa uhakika. Bila shaka mtaona itakapofika Desemba mwaka huu awamu ya pili ya mradi itakuwa imekamilika.”

Dkt. Biteko alisisitiza kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inathamini juhudi za wananchi wa Monduli katika kilimo na ufugaji:
“Rais Samia anawapenda sana wananchi wa Monduli. Amewapelekea mradi huu wa maji kwa sababu anataka mifugo yenu istawi. Ameahidi kuwa wafugaji nchini wawe daraja la juu kama wananchi wengine.”

Aidha, aliahidi kuwa serikali itaendelea kuwapatia nyenzo muhimu kwa maendeleo yao:
“Wanachohitaji wananchi ni maji, umeme na barabara. Rais Samia ameapa kuwapatia nyenzo hizo ili kufanikisha shughuli zenu za kila siku.”

Kuhusu huduma ya umeme, Dkt. Biteko alieleza kuwa vijiji vyote vya Wilaya ya Monduli tayari vimepata umeme na vitongoji vilivyosalia vitahudumiwa baada ya uchaguzi:
“Katika vitongoji 236, vitongoji 72 tayari vimepata umeme. Vilivyosalia vitapata huduma hiyo mara baada ya Uchaguzi Mkuu.”

Akijibu ombi la Mbunge wa Monduli, Freddy Lowassa kuhusu upatikanaji wa nguzo za umeme, alisema:
“Nguzo za umeme 20 alizoomba Mbunge, kuanzia Alhamisi hadi wiki inayokuja tutaanza kuona watu wa hapa wanapata umeme bila masharti yoyote. Katika maisha tunapimwa kwa kazi si kwa maneno.”

Kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, alisema:
“Muungano wa miaka 61 wa Tanganyika na Zanzibar ni wa kipekee duniani. Mataifa mengi yamejaribu kuungana lakini yameshindwa. Tanzania imeendelea kuwa Taifa moja lenye amani.”

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa naye alieleza furaha yake kwa wilaya hiyo kupata huduma ya maji:
“Maji ni uhai. Namshukuru Rais Samia kwa kuona umuhimu wa kusaidia pia mifugo kupata maji.”

Kwa upande wake, Mbunge wa Monduli, Freddy Lowassa alisema huduma hiyo ni ukombozi mkubwa kwa wananchi:
“Kwa miaka mingi maji yamekuwa kero kubwa katika Wilaya yetu. Kwa kupata mradi huu, tunaomba umpelekee shukrani zetu Rais Samia.”

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Monduli, Mhandisi Naville Msaki alifafanua kuwa mradi huo ulisanifiwa mwaka 2021 na hadi sasa umefikia asilimia 96 ya utekelezaji:
“Mradi huu utahudumia wananchi 8,867 na mifugo 24,000. Utagharimu shilingi bilioni 2.7 hadi kukamilika kwake.”

Uzinduzi huo umepokelewa kwa shangwe na matumaini makubwa kwa wananchi wa Esilalei na Monduli kwa ujumla.

0 Comments:

Post a Comment