Mchungaji "Komando Mashimo" Hukumiwa Kifungo cha Miaka Miwili Gerezani

 


Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, imemhukumu mchungaji Daud Nkuba maarufu kwa jina la Komando Mashimo, Nabii Nikaya, (Mchungaji Mashimo) kutumikia kifungo cha miaka miwili gerezani baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mawili kati ya matatu aliyokuwa akishtakiwa nayo.

Mashimo ametiwa hatiani kwenye mashtaka ya kuingia kwa jinai na kuharibu mali, huku akiachiliwa huru kwenye shtaka la kutishia kwa vurugu.

Mshitakiwa alikuwa anakabiliwa na mashtaka matatu ambapo upande wa Jamhuri umethibitisha makosa mawili dhidi yake na kushindwa kuthibitisha shtaka la kutishia kwa vurugu.

Hukumu hiyo ilitolewa leo Machi 18, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhan Rugemalila, baada ya upande wa Jamhuri kuthibitisha makosa dhidi ya mshitakiwa bila kuacha shaka yoyote.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Rugemalila alisema, "Nimeridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi watano wa upande wa Jamhuri na vielelezo, ambapo wameweza kuthibitisha pasipo kuacha shaka kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo mawili. Hata hivyo, mshtakiwa ameachiliwa huru kwa shtaka la tatu kwa kuwa upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha pasipo kuacha shaka kuwa alitenda kosa hilo."

Aidha, alisema, "Mshtakiwa katika kosa la kuingia kwa jinai, mahakama inakupa adhabu ya kwenda jela miezi sita, na kosa la kuharibu mali, mahakama inakutia hatiani na kukupa adhabu ya kwenda jela miaka miwili. Pia, mahakama inakuachia huru kwa kosa la kutishia kwa vurugu kwa sababu upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha shtaka dhidi yako. Hivyo, utatumikia kifungo cha miaka miwili gerezani."

Kabla ya kusomewa adhabu, mshitakiwa alipata nafasi ya kujitetea, ambapo aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwa sababu ana familia inayomtegemea.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Rhoda Kamungu, uliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa kama sheria inavyoelekeza, ili iwe fundisho kwake na kwa jamii nzima.

Awali, ilidaiwa kuwa, Novemba 22, 2023, mchungaji Mashimo alifanya uhalifu katika maeneo ya Mbezi Luis Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam, kwa kuingia kwa jinai katika ardhi inayomilikiwa na Frola Mwashaa. Aidha, aliharibu ujenzi wa nyumba iliyokuwa eneo hilo, kinyume cha sheria.

Pia, ilidaiwa kuwa, katika shtaka la tatu, alimtishia Ramson Vicent kwa vurugu.

0 Comments:

Post a Comment