Kamishna wa Uhifadhi Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Musa Nassoro Kuji, ametoa wito kwa maafisa na askari wa Hifadhi ya Taifa Burigi - Chato kuongeza juhudi za kuboresha na kuimarisha shughuli za uhifadhi na utalii, akisisitiza umuhimu wa ubunifu katika kufikia malengo ya serikali ya kukuza sekta ya utalii nchini.
Kamishna Kuji alitoa maelekezo hayo alipofanya ziara ya kikazi katika hifadhi hiyo, Machi 16, 2025, kwa lengo la kukagua hali ya utendaji kazi na kutoa miongozo ya kuboresha utalii na uhifadhi katika eneo hilo.
“Ongezeni ubunifu katika utendaji kazi ili kuboresha na kuimarisha shughuli za uhifadhi na utalii na kuongeza idadi ya watalii na mapato kufikia azma ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kufikisha idadi ya watalii milioni 5 na mapato ya dola bilioni 6 za kimarekani kwa mwaka wa fedha mwaka 2025,” alisema Kamishna Kuji.
Kamishna Kuji aliongeza kuwa ili kufikia malengo hayo, ni muhimu kuimarisha usimamizi wa rasilimali watu na kutumia mbinu za kisasa na ubunifu katika utendaji kazi. Alisisitiza kuwa kuboresha miundombinu, kuimarisha usalama na utoaji wa huduma bora ni moja ya njia muhimu za kuvutia watalii na kuhakikisha utalii unachangia kikamilifu katika Uchumi wa Taifa.
Akizungumza kuhusu hali ya hifadhi, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Simon Aweda, alimshukuru Kamishna Kuji kwa kutenga muda wa kukutana na watumishi wa hifadhi hiyo.
Kamishna Aweda alifafanua kuwa hifadhi inaendelea kutekeleza mikakati ya kuboresha miundombinu ya utalii, huku ikitilia mkazo usalama na ulinzi, kwani hifadhi hii inapakana na nchi tatu; Rwanda, Burundi na Uganda.
“Hifadhi yetu inazidi kuimarika kiusalama na ina nafasi kubwa ya kukua kiutalii kwani kuna fursa mbalimbali za uwekezaji wa kambi za watalii na hoteli, hivyo tunaendelea kutangaza fursa hizi ili kuongeza mapato ya serikali na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa,” alieleza Kamishna Aweda.
Hifadhi ya Taifa Burigi - Chato, inayopatikana katika Kanda ya Magharibi, inajivunia kuwa na wanyama adimu, ikiwa ni pamoja na Mbega Wekundu (Ashy Red Colobus Monkey), na ni maarufu kwa mchango wake mkubwa katika uhifadhi na kukuza sekta ya utalii. Kamishna Aweda aliongeza kuwa hifadhi hiyo inayo fursa kubwa ya kukuza utalii na kuwa kivutio cha kimataifa.
Ziara ya Kamishna Kuji katika Hifadhi ya Taifa Burigi - Chato ililenga kuhimiza juhudi za pamoja, ubunifu na ushirikiano katika kuboresha utendaji kazi wa hifadhi, ili kufikia malengo ya serikali na kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania kupitia sekta ya utalii.


0 Comments:
Post a Comment