CHADEMA Yamlima Barua Mchome. Mwenyewe Asema Anatafakari




Mchome Akosolewa na Uongozi wa Chadema Kulalamikia Maamuzi ya Katibu Mkuu.


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Mwanga, Lembruce Mchome, amesema maamuzi ya kukilalamikia chama hicho kwa Msajili wa Vyama vya Siasa yamechagizwa na kutokuridhishwa na majibu ya Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika.


 Mchome ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la CHADEMA, alibainisha hayo Machi 26, 2025, alipozungumza kuhusu uamuzi wake wa kupeleka malalamiko kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, akitaja hoja nne alizoziwasilisha mbele ya msajili baada ya kutokuridhishwa na majibu ya chama chake.


Akizungumzia malalamiko yake, Mchome alisema: "Barua hii nililiandika Machi 15, 2025, na ombi langu lilikuwa kumtaka Msajili achunguze kikao cha Baraza Kuu la chama kilichofanyika Januari 22, 2025. Nilimuomba achunguze kumbukumbu za kikao hicho kuanzia orodha ya wajumbe waliokuwepo, ajenda za kikao na mwenendo mzima wa kikao."


Aidha, alieleza kuwa alimuomba Msajili kutengua uteuzi wa wajumbe wote wa Kamati Kuu walioteuliwa kwenye kikao hicho pamoja na kutengua maamuzi yote yaliyofanywa na kamati kuu kuanzia Januari 22 hadi leo. Aliongeza: "Niliomba pia Msajili amuelekeze Katibu Mkuu, John Mnyika, kuitisha Baraza Kuu la chama ili tuweze kurudia zoezi hilo la uthibitishaji."


Hata hivyo, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kupitia barua ya Naibu Msajili, Sisty Nyahoza, ilitoa wiki moja kwa CHADEMA kujibu malalamiko ya Mchome. Nyahoza alisisitiza: "CHADEMA inatakiwa kutoa majibu kwa malalamiko haya kabla ya Machi 31, 2025."



Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, alizungumzia suala hili na kusema kuwa uteuzi wa wajumbe wa Kamati Kuu ulifuata kanuni na Katiba ya chama hicho na kwamba hakuna kilichovunjwa. Mnyika alisisitiza: "Uteuzi huu ulizingatia kanuni na katiba ya chama. Kinachofanyika ni sehemu ya mchakato wa kuondoa chama kwenye msitari wa 'No Reforms No Election' (hakuna uchaguzi bila mabadiliko)."


Saa chache baada ya uongozi wa CHADEMA Mkoa wa Kilimanjaro kumtaka Mwenyekiti wa Wilaya ya Mwanga, Lembruce Mchome, ajieleze, Mchome alithibitisha kupokea barua hiyo na kusema kuwa anatafakari hatua zitakazofuata. 


Alisema: "Kimsingi nimepokea barua hiyo leo (Machi 26, 2025) kutoka kwa Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Kilimanjaro ya kueleza shutuma dhidi yangu. Bado natafakari nini nifanye."



Katika barua ya Machi 26, 2025, ya Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema, Mchome alituhumiwa kukiuka maadili ya chama kwa mujibu wa katiba ya chama. 


Lema alieleza: "Ninakuandikia kwa mujibu wa katiba ya chama ya mwaka 2006 toleo la 2019 kuhusu maadili ya viongozi kifungu cha 10.1(viii), 10.2(ix) na maadili ya wanachama kifungu 10.3(iii)."


Barua hiyo ilieleza kuwa, kama kiongozi katika chama, Mchome alitakiwa kuonyesha mwenendo unaoakisi taswira ya chama kwa kuwa mkweli, mtiifu, na imara katika kutekeleza wajibu wake na ulinzi imara wa katiba ya chama. 


Aidha, barua ilisema kuwa Mchome alituhumiwa kutoa maneno yenye ukakasi na shutuma dhidi ya chama, ikiwa ni pamoja na barua yake ya kulalamikia akidi ya kikao cha Baraza Kuu cha Januari 22, 2025.


"Unajua wazi kuwa watu hawa ni maadui wa chama na ya kwamba kila wakati wanatutafutia makosa ili kukidhuru chama chetu. Lakini wewe kwa makusudi mazima umempasia mpira tena ndani ya kumi na nane dhidi yetu," ilisema barua hiyo.


Uongozi wa CHADEMA Mkoa wa Kilimanjaro ulimtaka Mchome apeleke utetezi wake kwa Katibu wa Mkoa ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya barua hiyo. 


Barua ilisema: "Kumbuka kwamba kitendo cha kutolea majibu yako kwa wakati uliopewa katika barua hii hakitazuia Baraza la Uongozi kuendelea na kutumia mamlaka yake kikatiba dhidi yako."


Hali ya kisiasa katika CHADEMA Wilaya ya Mwanga inazidi kuwa ya mvutano huku uongozi wa chama ukijaribu kudhibiti mivutano ya ndani inayozidi kuonekana.


0 Comments:

Post a Comment