Sakata la Kupotea kwa Mfanyabiashara Lachukua Sura Mpya: Polisi Waanza Uchunguzi, TRA Waibuka na Kukanusha Kuhusika

 


Sakata la kupotea kwa mfanyabiashara Daisle Simon Ulomi, mwenye umri wa miaka 43, limeendelea kuchukua sura mpya huku Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi wa kina huku Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imejitokeza na kukanusha kuhusika kwao na kupotea kwa mfanyabiashara huyo, ikisema taratibu za forodha hufanyika kwa mujibu wa sheria.


Tukio hili lilianza kusambaa mitandaoni kupitia ukurasa wa Boniface Jacob kwenye mtandao wa X, ambapo alichapisha ujumbe ulioeleza:

AMEPOTEA AMEPOTEA AMEPOTEA
"Hakurudi nyumbani kwake tangu alipoondoka kazini tarehe 11 Desemba, 2024."

Jina: DAISLE SIMON ULOMI
Umri: 43 miaka
Kazi: Mfanyabiashara

Mara ya mwisho alionekana akitoka ofisini kwake Sinza Kijiweni saa 6:00 mchana, akielekea Mbagala, Bandari Kavu kukagua kontena la mizigo yake kwa wito wa watu wa TRA."

Ujumbe huu ulizua taharuki, huku familia yake ikiendelea kumsaka bila mafanikio.

Polisi Waanza Ufuatiliaji
Jeshi la Polisi limethibitisha kupokea taarifa ya kutoweka kwa Daisle tarehe 12 Desemba 2024, baada ya familia yake kutoa taarifa rasmi katika Kituo cha Polisi Chang’ombe, Temeke. Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Muliro  Muliro, uchunguzi unaendelea kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali.

SACP Muliro alisema:

“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa kuhusu alipo mtu huyo kuwasiliana na kituo cha polisi kilicho karibu au mamlaka yoyote ya serikali.”

Simu ya Daisle ilionekana mara ya mwisho kuwa hewani tarehe 11 Desemba 2024, katika eneo la Temeke/Chang’ombe.



TRA Yakana Kuwa na Uhusiano
Katika hatua nyingine, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imejitokeza na kukanusha kuhusika kwao katika sakata hili. Kupitia taarifa rasmi, TRA ilisema:

“Kwa mujibu wa kumbukumbu zetu, Bw. Daisle Simon Ulomi alichagua kampuni ya wakala wa forodha ya TWENDE Freight Forwarders Limited kupitia barua yake ya tarehe 05 Desemba, 2024, kuwajibika kuondosha mizigo yake bandarini. TRA haijawahi kumuita wala kushirikiana naye moja kwa moja kwa jambo lolote.”

TRA ilisisitiza kuwa mchakato wa uondoshaji wa mizigo bandarini hufanyika kwa mujibu wa sheria, na suala la kupotea kwa mfanyabiashara huyo ni jukumu la Jeshi la Polisi.

“Pamoja tunajenga Taifa letu,” ilisema TRA kupitia Idara ya Elimu kwa Mlipa Kodi na Mawasiliano.

Ndugu na Familia Wanaendelea Kumtafuta
Familia ya Daisle inasema imepita vituo mbalimbali vya polisi bila mafanikio. Wito umetolewa kwa wananchi wenye taarifa kuhusu alipo mfanyabiashara huyo kuwasiliana na vyombo vya dola.

Sakata hili linaendelea kufuatiliwa kwa karibu huku polisi wakiahidi kuchukua hatua zote zinazohitajika ili kubaini ukweli.

0 Comments:

Post a Comment