"NADHARIA HEWA" KATIKA MBIO ZA UENYEKITI WA CHADEMA TAIFA NA JINSI UHALISIA ULIVYO (Illusion Vs Reality)



Na. Edward Kinabo


Nadharia kuu, lakini hewa,  iliyotawala mbio za Uenyekiti wa Chadema Taifa, ni baadhi ya wana-Chadema na mashabiki wa Chama hiki, kudhani kuwa Chadema imekosa na kwa hiyo, inahitaji kupata mwenyekiti mkali (radical), wa kuweza kuendesha siasa ngumu, mwenye misimamo mikali, na mwenye ujasiri wa kupambana na dola. Kwamba, mwenyekiti wa namna hiyo, ndiye atakayekiwezesha Chama kukomesha wizi wa kura kote nchini. Kwamba, huyo ndiye atawezesha ushindi na kuiondoa CCM madarakani. 



Na kwamba huyo ndiye mwenye ujuzi na miujiza ya kuingiza watu barabarani. Ndiye mwenye upako wa kuwaambia Watanzania waandamane halafu kweli wakaandamana! 


Hata hivyo, tofauti kabisa na nadharia hiyo (illusion), uhalisia na ukweli wa mambo (reality) upo hivi:


1. Tayari Chadema, imeshajaribu mara kadhaa kuendesha hizo siasa ngumu (za kuingiza watu barabarani), lakini hazijafanikiwa vya kutosha, na wakati mwingine, viongozi wa Chadema, kwa pamoja, wamelazimika kuongozwa na busara ya ama kuepuka kufanya"maandamano yasiyowezekana" au kuepuka kusababisha maafa na umwagaji wa damu za Watanzania usio na tija ya moja kwa moja katika kuleta mabadiliko yanayotafutwa.


2. Ni ukweli usiopendeza kuwa, kukwama kwa siasa ngumu, pamoja na hofu iliyotokana na tishio la kujaribu siasa  ngumu, kumewahi kusababisha baadhi ya viongozi wetu kulazimika kukimbia nchi wakihofia usalama wao.


3. Uwenyekiti wa Chama Taifa haujawahi kuwa kikwazo wala kizuizi dhidi ya Chama kufanya  siasa kali au siasa ngumu. Maamuzi yote ya Chadema juu ya siasa gani zifanyike au hatua gani ichukuliwe katika kukabiliana na Chama Dola cha CCM, yamekuwa yakiamuliwa kwa pamoja katika vikao vya juu vinavyojumuisha viongozi wa sampuli zote, wakiwemo wale wanaodhaniwa ni wapole sana na wale wanaodhaniwa kuwa ni wakali na majasiri sana.


4. Aidha, viongozi wowote wale ndani ya Chadema, wanaodhaniwa kuwa wana miujiza ya kuikomboa nchi kwa kutumia siasa ngumu, bado wangeweza japo kuonesha mfano wa kuishinda CCM kwa kutumia siasa ngumu na mbinu mpya kutoka kwenye maeneo wanayotokea au waliyohusika moja kwa moja kuongoza kampeni na ulinzi wa kura. Hata hivyo, ukweli unathibitisha kuwa siasa za mabavu za CCM na Serikali yake, bado zimeendelea kuipiga Chadema kote nchini, bila kujali pale kuna Kiongozi mkali sana au mpole sana.


5. Ukweli mkubwa kuliko wote ni kwamba siasa ngumu na kali (radical politics) hazihitaji tu kiongozi mkali bali zinahitaji zaidi jamii yenye hulka, mwamko na ujasiri wa kutosha wa kudai haki zake (radical/aggressive society), lakini kwa bahati mbaya, Watanzania, kwa ujumla wao, bado hawafanani na jamii ya na namna hiyo. 


Kwa hiyo, shida si ukali wala upole wa uwenyekiti bali shida ni jamii yenyewe. Ni kwasababu ya jamii hiyo hiyo, ndiyo maana Mwenyekiti wa sasa wa Chadema Taifa, Mhe Freeman Mbowe, alijikuta akiandamana peke yake na watoto wake, kupigania haki za wananchi wanaotekwa, kupotezwa na kuuwawa.


6. Pamoja na changamoto zote hizo za kuwa na jamii iliyopoa au iliyopooza, bado Chadema imefanikiwa kufanya kazi kubwa ya kujenga uelewa na kuhamsha jamii katika kupigania haki na maendeleo yao.Tarime, Karatu, Arusha, Hai, Mwanza mjini, Mbeya mjini, Tunduma n.k ni baadhi tu ya sehemu kadhaa za nchi hii ambazo Chadema imefanikiwa kujenga nguvu na ujasiri wa umma katika kupigania haki zao kwa ujasiri wa hali ya juu.


7. Hata hivyo, kwa kadri Chadema ilivyokuwa inapiga hatua katika kujenga mwamko na nguvu ya umma, ndivyo na Chama Dola nacho kinavyozidi kuachana kabisa na siasa, na kuzidi kutumia nguvu kubwa zaidi za dola katika kuminya demokrasia  na kusambaratisha madai ya haki. 


8. Kwasasa, matumizi ya nguvu za dola yamezidi na kukithiri hadi kufikia kiwango ambacho ni ngumu sana kwa Chama cha Siasa kuweza kukabiliana nayo kisiasa. Na kwa kuwa wana Chadema wote hatuamini katika siasa za uasi, basi inakuwa ni uonevu na ukatili wa hali ya juu kudhania kuwa Chadema haipati ushindi kwasababu uongozi uliopo ni dhaifu au umeishiwa mbinu. Chadema ni chama siasa,  imejengwa na kuwa Chama imara cha siasa - Chadema haiwezi kuwa kikosi cha kijeshi.


9. Kwa hiyo, ni maoni na mtazamo wangu kuwa,mabadiliko katika nchi hayawezi kupatikana kwa nadharia ya mkato ya kudhania ukali wa Kiongozi pekee unatosha kushindana na nguvu kubwa za dola, bali yatapatikana kwa kuendelea kutekeleza mkakati mpana na endelevu wa kuhamsha umma na kuujengea ujasiri wa kuweza kuona na kuchukua hatua madhubuti zaidi za kupigania katiba, sheria bora na tume huru ya uchaguzi. Kwa vyovyote vile, kazi hiyo haiwezi kuwa ya mkato wala ya kuhitaji ukali wa ghafla ili kuwabadili wananchi, bali inahitaji mkakati makini, jumuishi na shirikishi zaidi utakaowajengea wananchi uelewa,utayari na uchungu wa kutosha kudai demokrasia na uhuru wa kuiongoza nchi yao kupitia chaguzi huru na za haki.


10. Aidha, kama ilivyoazimiwa na Kamati Kuu ya Chadema, ni maoni na mtazamo wangu pia,  kwamba kazi kubwa na endelevu ya kuhamsha umma, inapaswa kwenda sambamba na kazi nyingine kubwa na endelevu ya kufanya "strategic advocacy engagements" inayolenga wadau wa ndani ya nchi pamoja na taasisi na majukwaa ya kimataifa ili kuweza kupata uungwaji mkono mkubwa, na hivyo kuongeza shinikizo kwaajili ya kulegezwa kwa vikwazo vya kidemokrasia vilivyowekwa dhidi ya vyama vya upinzani hapa nchini. Kazi hii nayo si ya mkato lakini haina budi kufanyika.

0 Comments:

Post a Comment