Mbowe Aipinga Jeshi la Polisi, Wananchi Wazidi Kushinikiza Uachiliaji wa Waliotekwa

 Mbowe Aipinga Jeshi la Polisi, 

Wananchi Wazidi Kushinikiza Uachiliaji wa Waliotekwa





Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ameibuka na kauli kali akipinga tuhuma za Jeshi la Polisi dhidi ya chama chake, akilieleza kama "shambulio la kizushi na chuki." 

Akizungumza kupitia ukurasa wake wa kijamii wa X, Mbowe amehoji msingi wa madai ya Jeshi la Polisi kuwa viongozi wa CHADEMA walikuwa wanapanga njama za vurugu kupitia mkutano wa Zoom, akisisitiza kuwa chama chake hakijahusika na kikao hicho.


"Hili ni shambulio lingine la kizushi na chuki dhidi ya CHADEMA na viongozi wake," alisema Mbowe, akiongeza kuwa tuhuma hizo ni kisingizio cha kuendelea kuwakamata na kuwatesa wanachama wa CHADEMA kwa kutumia taarifa za uongo. 


Mbowe aliendelea kusisitiza kuwa "utekaji ni uhalifu" na hauwezi kuwa sehemu ya mkakati wa kulinda amani ya nchi, huku akiwataka viongozi wa serikali kueleza walipo viongozi wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) waliopotea.



Kwa upande mwingine, msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, amesisitiza kuwa jeshi hilo linaendelea na uchunguzi kuhusu kupotea kwa viongozi wa BAVICHA, lakini pia alitoa onyo kali kwa yeyote anayepanga kuvuruga amani kwa kutumia mbinu za uhalifu. 



Misime alibainisha kuwa Jeshi la Polisi limepata taarifa za uhakika kuhusu njama za kuhamasisha vurugu kupitia mitandao na kikao cha Zoom, na kuonya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wahusika.


Hata hivyo, kauli hizi zimeongeza shinikizo kutoka kwa wanasiasa, wanaharakati, na wananchi wa kawaida, ambao wameungana kushinikiza Jeshi la Polisi kuwaachia watu wanaodaiwa kutekwa. Wengi wanaeleza kuwa wanataka uwazi zaidi na hatua za haraka za serikali kuhakikisha watu waliopotea wanapatikana na kuachiliwa.


"Tunataka serikali itueleze, watu hawa walipo," alisema mwanaharakati mmoja wa haki za binadamu, akisisitiza kuwa suala la utekaji halipaswi kufumbiwa macho. Mmoja wa wanasiasa wa upinzani naye aliongeza, "Hii ni vita ya haki za binadamu. Wananchi wanataka majibu, na wanahitaji kuona haki ikitendeka."


Wananchi wa kawaida pia hawajaficha hisia zao, wakilalamika juu ya ongezeko la hofu miongoni mwao kutokana na matukio ya utekaji. "Hatuwezi kuendelea kuishi kwa hofu. Tunahitaji kujua watu wetu walipo na kwa nini wanachukuliwa," alisema mmoja wa wakazi wa Arusha. 


Hali hii inaashiria kuzidi kwa presha ya kisiasa nchini, huku kukiwa na wito wa kuimarishwa kwa uwajibikaji na uwazi kutoka kwa vyombo vya dola ili kulinda haki za raia na kuleta utulivu wa taifa.

0 Comments:

Post a Comment