Dkt. Nchimbi Aagiza Kuachiwa Huru kwa Viongozi wa CHADEMA Mbeya



Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amemuagiza Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo, kuwaachia huru viongozi wote wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanaoshikiliwa na polisi Jijini Mbeya. 


Agizo hili lilitolewa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Wilayani Geita, mkoani Geita, wakati akizungumza na wakazi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro.


Dkt. Nchimbi alisema, "Nia yetu ni kujenga Taifa moja lenye amani. Ikiwa kuna maeneo ambapo kuna tofauti kati yetu au kati ya vyama, ni bora tukakaa chini na kujadili. Tunahitaji kuwa na Taifa tulivu na yenye mshikamano." 


Aliweka msisitizo kwamba Rais Samia Suluhu Hassan anapendelea kutatua migogoro kwa njia ya mazungumzo badala ya matumizi ya nguvu.


Katika hotuba yake, Dkt. Nchimbi alieleza jinsi alivyofanya jitihada za kuzungumza na viongozi wa vyama vingine kuhusu hali hiyo. 


Alibaini kuwa mmoja wa viongozi wa CHADEMA alikuwa amekamatwa, jambo ambalo lilimfanya kutumia nafasi hiyo kumtaka Naibu Waziri Sillo kuzungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani ili kuhakikisha viongozi hao wa CHADEMA wanaachiwa huru. 


Dkt. Nchimbi aliongeza, "Tuache nafasi kwa wanasiasa kwanza tuzungumze kabla vyombo vya sheria havijachukua hatua. Tunataka kujenga taifa moja lenye umoja na amani. Ikiwa kuna makosa, ni bora tukae na kujadili."


Katika ziara yake ya siku tatu mkoani Geita, Dkt. Nchimbi ameambatana na wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM, akiwemo Ndugu Issa Haji Usi Gavu (Katibu wa NEC - Oganaizesheni), Ndugu Amos Gabriel Makalla (Katibu wa NEC - Itikadi, Uenezi na Mafunzo), na Ndugu Rabia Hamid Abdalla (Katibu wa NEC - Siasa na Uhusiano wa Kimataifa). Kesho, anatarajiwa kuzungumza na wananchi mjini Geita katika mkutano mkubwa wa hadhara utakaofanyika katika Uwanja wa Nyankumbu.

0 Comments:

Post a Comment