Mahakama ya juu zaidi nchini Afrika Kusini imemzuia rais wa zamani Jacob Zuma kuwania ubunge katika uchaguzi mkuu utakaofanyika wiki ijayo. Mahakama ya Kikatiba iliamua kwamba kifungo chake cha miezi 15 jela kwa kupuuza agizo la mahakama - uhalifu chini ya sheria za Afrika Kusini - kilimfungia.
Zuma alipatikana na hatia mwaka wa 2021 kwa kukataa kutoa ushahidi wake katika uchunguzi wa ufisadi wakati wa uongozi wake uliokamilika mwaka wa 2018. Amekuwa akifanya kampeni kupitia chama kipya cha Umkhonto weSizwe (MK) baada ya kutofautiana na chama tawala cha African National Congress (ANC).
Katibu mkuu wa MK, Sihle Ngubane, amesema chama hicho kimesikitishwa na uamuzi huo, lakini hautaathiri kampeni za chama na uso wa Zuma utaendelea kubaki kwenye karatasi ya kupigia kura katika uchaguzi wa tarehe 29 Mei.
"Bado ni kiongozi wa chama. [hukumu] haiathiri kampeni yetu hata kidogo," alisema Ngubane.
Wananchi wa Afrika Kusini huvipigia kura vyama vya siasa, huku wagombea walio juu ya orodha zao wakipata viti vya ubunge kulingana na idadi ya kura ambazo chama kinapata. Tume ya uchaguzi ilisema jina la Bw. Zuma sasa litaondolewa kwenye orodha ya wagombea ubunge wa MK, huku ikithibitisha kwamba sura yake itasalia kwenye karatasi za kupigia kura, sambamba na nembo ya chama chake.
Wanachama wa MK waliimba na kucheza nje ya mahakama wakimuonyesha Zuma kama mwathiriwa, huku wale waliokuwa ndani - wengine wakiwa wamevalia mavazi ya kitamaduni ya Kizulu - walikaa kimya huku Jaji Leona Theron akisoma hukumu hiyo kwa kauli moja.
Zuma bado hajatoa maoni yake kuhusu uamuzi huo. Wafuasi wake walizua ghasia baada ya kupelekwa jela mwaka wa 2021, na baadhi ya viongozi wake walitishia ghasia iwapo mahakama ingemzuia kugombea ubunge.
Hata hivyo, maafisa wa MK wamebadili kauli yao wakisema lengo la chama ni kupata theluthi mbili ya kura ili katiba ya Afrika Kusini ibadilishwe, na Zuma arejeshwe mamlakani.
Mahakamani, mawakili wake walidai kwamba kwa sababu aliachiliwa baada ya miezi mitatu jela na mrithi wake, Rais Cyril Ramaphosa, kifungo chake kilichosalia kilifutwa. Lakini mahakama ilikataa, ikisema urefu wa muda aliokaa gerezani haukuwa na maana.
Katiba ya Afrika Kusini inamzuia mtu yeyote aliyehukumiwa kifungo cha miezi 12 jela, bila chaguo la faini, kuhudumu bungeni ili kulinda uadilifu wa "utawala wa kidemokrasia" ulioanzishwa baada ya kumalizika kwa mfumo wa ubaguzi wa rangi mwaka 1994, Jaji Theron alisema.
0 Comments:
Post a Comment