Kimbunga 'Hidaya' kinazidi Kusogea Pwani

 


Serikali ya imethibitisha kuwa kimbunga ‘Hidaya’ kinaendelea kusogea kuelekea maeneo ya  pwani ingawa kasi ya kimbunga hicho inapungua.


Msemaji mkuu wa serikali ya Tanzania, Mobhare Matinyi amesema hayo wakati akiongea na vyombo vya habari.


“Mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa baharini inaonesha uwezekano wa kasi ya kimbunga hicho kupungua zaidi ndani ya saa 12 zijazo, jambo ambalo ni taarifa njema huku kikiendelea kusogelea pwani ya Tanzania. Kimbunga hiki kinatarajiwa kuendelea kuwepo hadi tarehe 5 Mei na kitaendelea kupungua nguvu kwa mujibu wa vipimo vya wataalamu wetu.” Alifafanua.


Msemaji huyo mkuu wa serikali ameeleza zaidi kuwa “Uwepo wa kimbunga Hidaya karibu na pwani ya nchi yetu kunatarajiwa kutawala na kuathiri mfumo wa hali ya hewa hapa nchini ikiwa ni pamoja na kusababisha vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani ikiwa na pamoja na kisiwa cha Mafia, Dar es Salaam, pamoja na mikoa ya Tanga, Morogoro na visiwa vya Unguja na Pemba. Tayari vipindi vya mvua na upepo vimeanza katika mikoa ya Pwani na Lindi”.


Amewataka wakazi wa maeneo yaliyotajwa kuathirika na kimbunga ‘Hidaya’ kuendelea kufuatilia taarifa za mamlaka ya hali ya hewa na maelekezo ya taasisi za serikali na pia kuchukua tahadhari.


Mara ya mwisho Tanzania Bara kupigwa kimbunga kikali ilikuwa mwaka 1952 wakati huo ikiitwa Tanganyika na kuathiri eneo la mkoa wa Lindi. Kabla ya hapo kimbunga kingine kikali kiliipiga Zanzibar mwaka 1872.


Katika miaka ya karibuni kulitokea kimbunga Jobo mwaka 2021 ambacho hakikuwa na athari kubwa zaidi ya mvua za wastani na upepo. Hali kama hiyo ilitokea mwaka 2019 wakati wa kimbunga Kenneth huko mkoani Mtwara lakini kilikuwa na madhara makubwa nchini msumbiji na Malawi.

0 Comments:

Post a Comment