Helikopta Iliyombeba Rais wa Iran Yahusika Katika Ajali, Vyombo vya Habari vya Serikali Vinaripoti
Vyombo vya habari vya serikali vinaripoti kuwa Rais wa Iran Ebrahim Raisi alikuwa kwenye helikopta ambayo ilitua kwa dharura siku ya Jumapili.
Helikopta hiyo pia ilisemekana kumbeba Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amirabdollahian.
Waziri wa Mambo ya Ndani alisema waokoaji bado wanajaribu kufika eneo la ajali kutokana na hali mbaya ya hewa.
Hali ya waliokuwemo ndani ya helikopta hiyo bado haijajulikana, na hakuna mawasiliano yaliyofanywa.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani, Rais Raisi alikuwa akielekea katika mji wa Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran, baada ya kurejea mpakani na Azerbaijan ambako alifungua mabwawa ya Qiz Qalasi na Khodaafarin.
Ukungu mkubwa unafanya msako kuwa mgumu katika eneo ambalo inadhaniwa kuwa huenda helikopta hiyo ilitua, kulingana na ripota wa shirika la habari la Fars. Alisema mwonekano katika eneo la milima na misitu ulikuwa chini hadi takriban mita tano tu. Eneo hilo ni kama kilomita 50 kaskazini mwa Tabriz.
Ahmad Alirezabeigi, Mbunge wa Iran kutoka mji wa Tabriz, amewaambia waandishi wa habari mjini Tehran kwamba waokoaji bado hawajapata eneo la helikopta iliyombeba rais na waziri wa mambo ya nje.
Aliongeza kuwa helikopta nyingine mbili katika msafara huo zilitua salama. Kanda za video zimeibuka kwenye televisheni ya taifa zikionyesha waumini wakimuombea afya rais katika mji mtakatifu wa Mashhad.
Rais wa Iran Ebrahim Raisi ni Nani?
Ebrahim Raisi, mwenye umri wa miaka 63, alichaguliwa kuwa rais katika jaribio lake la pili mwaka wa 2021. Anaonekana kama mhubiri mwenye msimamo mkali na anachukuliwa kuwa mrithi wa Ayatollah Khamenei siku moja, kiongozi mkuu wa nchi hiyo tangu 1989.
Mnamo mwaka wa 2019, Kiongozi Mkuu alimteua kwenye nafasi yenye nguvu ya mkuu wa mahakama.
Raisi pia alichaguliwa kuwa naibu mwenyekiti wa Bunge la Wataalamu, baraza la makasisi lenye wanachama 88 walio na jukumu la kumchagua Kiongozi Mkuu ajaye.
0 Comments:
Post a Comment