WADAU WA UTALII DUNIANI WAVUTIWA KUWEKEZA NCHINI TANZANIA

 

WADAU WA UTALII DUNIANI WAVUTIWA  KUWEKEZA NCHINI TANZANIA



Kampuni kubwa zinazojishughulisha na masuala ya utalii duniani zimevutiwa kuwekeza nchini Tanzania katika huduma za malazi, usafirishaji na  utangazaji utalii. 


Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki (Mb) katika Maonesho ya Utalii ya ITB yanayoendelea jijini Berlin Ujerumani.



“Nimefurahi kukutana na kampuni kubwa ya TUI (TUI Group) yenye Makao Makuu nchini Ujerumani ambayo ina hoteli zaidi ya 400 duniani, meli za kitalii 16, mashirika ya ndege matano na zaidi Mashirika 1,200 ya usafiri”  Kairuki amesisitiza.

 


Amefafanua kuwa kampuni hiyo imewekeza Zanzibar na hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu itazindua hoteli yao ya tisa lakini kwa upande wa Tanzania Bara inaendelea kufungua safari za ndege ili kuleta watalii katika hifadhi zilizopo nchini Tanzania.


Aidha, Kairuki amekutana na kampuni inayosafirisha watalii zaidi ya milioni 1.2 duniani yenye Makao Makuu  Marekani  na Puertoriko ambayo imeonyesha utayari na kuanzia mwezi Mei mwaka 2024 italeta Wakala wa Usafirishaji zaidi ya 40 kutembelea maeneo mbalimbali nchini Tanzania.


Waziri Kairuki pia amekutana na kufanya mazungumzo na Kampuni ya Kimataifa Kusafirisha Watalii ya Expedia Group pamoja na kampuni kutoka Slovakia ambayo inapeleka watalii duniani kwa zaidi ya asilimia 85 kutoka nchini humo na ina matangazo katika luninga zao na kujadili namna ya kushirikiana katika kuandaa matangazo ya vivutio vya utalii.



Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Damas Mfugale amesema ushiriki wa Tanzania kwenye Maonesho hayo ni chachu ya kuongeza idadi ya watalii nchini.

0 Comments:

Post a Comment