Andiko la Askofu Bagonza kumhusu hayati Lowassa na Aliyemteua

Andiko la Askofu Bagonza kumhusu hayati Lowassa na Aliyemteua 

Hayati Edward Lowassa enzi za uhai wake akiwa na mke wake, Regina 


EDWARD KAMA EDWARD
Jana 17/2/2024 tumemzika EDWARD Lowasa nyumbani kwao Monduli. Miaka 40 iliyopita tulimzika EDWARD Sokoine katika eneo hilo hilo la Monduli.  Tulivyomzika Edward yule, ndivyo tumemzika Edward huyu. Jina “Edward” lina maana kubwa katika eneo hilo hata kama siijui.
Yalikuwa ni mazishi yenye hadhi. Usingejua kama ni ya Waziri Mkuu Mstaafu. Waziri Mkuu yeyote aliye madarakani bado yangemfaa. Yaliandaliwa chini ya Uenyekiti wa Waziri Mkuu aliye madarakani - Majaliwa Kassim Majaliwa. Kazi nzuri.
Miongoni wa waliohudhuria mazishi ni Huzuni, fahari, furaha, aibu na fundisho.
Nilitafakari haya;
1. Edward aliondoka Monduli mara ya mwisho akiwa amesimama. Amerudi amelala. Kulala na kusimama; Yote mawili yana nguvu na hadhi sawa. Tuwe wanyenyekevu.
2. Edward ameliunganisha taifa letu japo kwa siku moja. Wote tulikaa kwa adabu na utulivu na kusahau kwa muda tofauti zetu. Wote tulitumia “washroom” zile zile bila kubaguana. Kumbe inawezekana?
3. Tangu afariki dunia hata mitandao inasema uzuri wa Edward. Imejikita kuwazodoa wanaodhaniwa ni wabaya wa Edward. Fupisheni hukumu zenu juu yao. Yawezekana aliisha wasamehe.
4. Mishangao yangu: Kutowaona niliodhani wangekuwepo. Kuwaona niliodhani hawawezi kuwapo. Kupopoa historia ya Edward iliyobeba haiba yake ya MAAMUZI MAGUMU.
5. Mazishi ya Edward Sokoine yalihudhuriwa na Oliva Tambo (Rais wa ANC ya wakati huo) na Alfred Nzo (Katibu Mkuu wa ANC wakati huo). Wageni wa nje waliohudhuria mazishi ya Edward Lowasa ni magavana wa Kimasai kutoka Kenya.
6. Ilipigwa mizinga: Mimi nilihesabu 16, jirani yangu akahesabu 17. Jirani wa upande wa pili akasema ilitakiwa 21.
Timu ya wana itifaki wa serikali na jeshi wakawatahadhalisha wenye mimba; wakasahau tuko wajinga wengi tusiojua mizinga 16/17 au 21 ina maana gani? Akifa mwingine mtueleze tafadhali!
*7. Freeman Mbowe  “aliiba onyesho” msibani. Alipata fursa kusalimia kama mwana familia. Akainadi Chadema. Akaboresha historia ya Edward. Mama akaikamilisha. Siku yenye huzuni ikaisha vizuri. Tukasikia makofi msibani.*
8. Tulipomzika Edward Sokoine, tulizika darasa la uongozi. Kwa kumzika Edward Lowasa, twaweza kuwa tumezika maabara ya uongozi. Mmoja aliamini katika ufukara mtakatifu. Mwingine katika utajiri-uzalendo. Tusihemuke, tutafakari.
9. Edward huyu ameacha msiba kuliko msiba wa kifo chake. Tuna kizazi cha viongozi vijana na wazee vijana. Hawa Mungu wao ni tumbo na mbingu yao ni madaraka. Upo uhusiano wa matumbo yao na dhamana waliyopewa: Matumbo yao yanapanuka wakati dhamana na taasisi zao zinakonda. Hawana kiu ya haki tena.
10. Monduli ilikuwa ndogo siku ya mazishi. Msiba ukahamia kwenye ng’ombe. Watu walizoea kula nyama alipokuwa hai. Wamekula zaidi alipokufa. Tupo ambao hatukusikia njaa pamoja na kutokula. Kwaresima ya 2024 tutaikumbuka kwa kushinda njaa tukikuzika. Fredy Lowasa umuenzi babako daima kwa kuwapa watu nyama walizozizoea alipokuwa hai.
HITIMISHO:
Nilitamani mmoja toka familia ya Edward Sokoine aongee na kutufariji.
*Nilitamani aliyemteua kuwa Waziri Mkuu atusalimie. Haikutokea. Ukisikia msiba, hiyo ndiyo maana yake. Ukipenda, mnyime mengine lakini ni muungwana sana. Alihudhuria.*
Tumalize matanga, maisha yaendelee.

0 Comments:

Post a Comment