WIZARA NA TAASISI ZATAKIWA KUCHUKUA HATUA KUKABILIANA NA MAAFA

 WIZARA NA TAASISI ZATAKIWA KUCHUKUA HATUA KUKABILIANA NA MAAFA 

Na Mwandishi wetu- Dodoma

Wizara na Taasisi za Serikali zimetakiwa kuendelea kuchukua hatua katika kujiandaa na kupunguza madhara yanayotokana na maafa hususani katika kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha nchini.


Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt. Salim Manyata Jijini Dodoma wakati akifungua Kikao Kazi cha Wataalam cha maandalizi ya kuandaa Mpango wa Hatua za Kuchukua katika Kuzuia na Kupunguza madhara ya mafuriko katika mito nchini.
Kapteni  Emmanuel Lyimo  kutoka Idara ya  Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu  akiwasilisha namna  Tanzania inavyochukua hatua katika kukabiliana  na maafa wakati wa kikao kazi cha Wataalam cha maandalizi ya kuandaa Mpango wa Hatua za kuchukua katika Kuzuia na Kupunguza madhara ya mafuriko katika mito nchini kikao kilichofanyika Jijini Dodoma.

Mkurugenzi huyo amesema kikao hicho kimefanyika kwa wakati muafaka katika kuelewa hatua madhubuti za kuchukua kwaajili ya kupunguza hatari za mafuriko ikizingaitwa mabadiliko ya mienendo ya hali ya hewa mara kwa mara pamoja na ongezeko la kasi na ukali wa matukio ya hali ya hewa.

“Kikao hiki kimekuja wakati sahihi hususani wakati huu nchi inapitia katika wakati wa mvua nyingi zinazosababisha mafuriko na kuleta madhara makubwa. Ni fursa kwetu kuchanganya maarifa yetu, kushirikiana kimawazo, na kujenga njia mbele inayojumuisha mawazo bora, teknolojia na njia zinazoshirikisha jamii ili kujenga uthabiti dhidi ya athari za mafuriko,”Amesema Dkt. Manyata.

Pia ameeleza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa ya Mwaka 2004 na Sheria ya Usimamizi wa Maafa, Na. 6 ya mwaka 2022 inaratibu na kusimamia masuala ya maafa nchini.

“Ofisi ya Waziri Mkuu na imeendelea kuchukua hatua za kupunguza madhara kwa kuhakikisha usimamizi na uratibu wa maafa na huduma za dharura zinatolewa kwa wakati kwa kuzingatia mipango, miongozo na mikakati ya kitaifa na kisekta,”Amebainisha.

Aidha ametoa wito kwa washiriki hao kubadilishana uzoefu katika kupunguza madhara ya mafuriko katika mito akisema kupitia jitihada za pamoja ili kuendeleza mikakati ambayo si tu inapunguza athari za mafuriko ya mito pia inaweka msingi wa Tanzania imara na yenye uwezo wa kubadilika.


(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

0 Comments:

Post a Comment