RC BABU AZINDUA TWENZETU KILELENI, AIPONGEZA ZARA ADVENTURES



Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, ameipongeza  Kampuni ya uwakala wa utalii ya ZARA Tanzania Adventures kwa jitihada zake katika kuendeleza utalii na kuhifadhi mazingira ya Mlima Kilimanjaro huku ikihakikisha wapanda mlima wanakuwa salama kwa kuingia makubaliano na kampuni ya ndege za uokoaji ya Kili MedAir.

 
Aidha ameipongeza kampuni hiyo kwa uzalendo walioonyesha kwani wamekuwa wakishiriki kupandisha watu kwenda kusherekea uhuru kwenye kilele cha mlima huo mrefu kuliko yote Afrika kuanzia mwaka 2008 ambapo mwaka huu wameanza  kampeni ya kuhakikisha kila mtu anapanda mti kabla ya kuanza kupanda mlim huo.



RC, Babu aliyasema leo Novemba 4,2023 wakati akizindua kampeni ya "Twenzetu Kileleni Kilimanjaro" yenye lengo la kuhamasisha wananchi kijitokeza kupanda mlima Kilimanjaro kwa ajili ya kusherekea miaka 62 ya uhuru.

Mkuu wa Mkoa aliweka msisitizo katika kuongeza jitihada za kuboresha shughuli za utalii na kuanzisha mikakati inayolenga kuimarisha usimamizi wa mazingira ya eneo hilo adimu kwa  ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali.

"Nichukue nafasi hii kukupongeza dada yangu Zara (Zainab Ansell) kwa moyo wako wa upendo wa kizalendo wewe kwa sababu unasimamia sana jambo hili," alisema mkuu wa mkoa Babu na kuongeza.

" Niseme kwamba kipindi kile tumepata matatizo ya moto kwenye mlima wetu wa Kilimanjaro ulikuwa mstari wa mbele kusaidia na makampuni mengine yakaiga kifanya kazi hiyo.

"Serikali imedhamiria kuhakiisha utalii wa Tanzania unakimbia hapa ulipo na unaenda mbele zaidi. Filamu ya The Royal  Tour imeleta mafanikio makubwa nchini mwetu na hasa kwenye suala zima la utalii.

"Ukiacha suala la kwenda mbugani lakini mlima kilimanjaro umepiga hatua kubwa ya kutembelewa na watalii wengi. serikali inashirikiana na sekta binafsi kupitia mpango wetu wa PPP (Public Private Patnership) katika kufikia malengo ya serikali.

"Kampuni inayoshiriiana na ZARA ya KiliMedAir imesaidia kutuondoa kwenye jambo tulilokuwa tunashughulikia kwa muda mrefu la watalii wanaopanda mlima kilimanjaro wakipata dharura wanashindwa kupata huduma kwa haraka,".

 
Jumla ya watu 320 wanatarajiwa  kupanda mlima mwaka huu, Mkuu wa Mkoa alipongeza jitihada za ZARA Adventure itakayopandisha watu 200  pamoja na kampuni nyingine mbili zitakazopandisha watu 150 kwa kuwa sehemu ya mafanikio ya shughuli hizi.

Mkuu wa Mkoa, akitoa mwito kwa wananchi kushiriki katika kusherehekea miaka 63 ya uhuru wa Taifa kwa kushiriki katika tukio hili muhimu kupitia kampeni ya wiki ya  'Twenzetu Kileleni Kilimanjaro' itakayoanza Desemba 4,2023.


Aidha, Mkuu wa Mkoa alipongeza  kampuni ya ZARA Tanzania Adventures katika kuhamasisha upandaji wa miti na ushiriki katika kampeni za kuhifadhi mazingira. 

"Ndugu zangu miaka ya nyuma mlima Kilimanjaro ulikuwa ukiutizama wakati mawingu hayapo ulikuwa umejaa barafu ya kutosha mpaka chini leo barafu vipande vipande kwasababu tunaharibu mazingira," alisema RC Babu na kuongeza.

"Sasa wale wote waliosema tutaungana kwenye kampeni tutahakikisha tunapanda miti ambapo nikupongeze mama ZARA umesema vizuri  kila mtalii anayekuja nchini kwetu nchi yetu tumuombe apande mti. Awe mtalii wa ndani au wa nje nje apande mti.

"Na sisi kampeni yetu ya mkoa barabara zote za TARURA na TANROAD zote lazima zipandwe miti upande wa kulia na kushoto na mwaka huu tunaanza kupanda kuanzia Biko unapoingia mkoa wa Kilimanjaro.

"Tunaenda kufanya kampeni  ya upandaji miti kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, hadi tarafa wao watakuwa walizi wa kutunza hiyo miti iende mpaka Same, Mwanga ikifika njia panda inaenda kuungana na Moshi kwa upande mwingine Taveta,".


Kwa upande wa Mkurugenzi wa kampuni ya, ZARA Adventure, Zainab alitoa wito kwa Watanzania wote kushiriki madhimisho wa wiki ya 'Twenzetu kileleni' kwa  kupanda mlima huku akiwataka kushirikiana katika zoezi la kupanda miti kabla ya kuanza kupanda mlima. 

 "Tukiweza kushirikiana pamoja tunaweza, tutakuwa na zoezi la kupanda miti kabla ya kupanda mlima kuonyesha kwamba tunaweza kulinda mazingira na mlima wetu. Na sisi kama ZARA Tanzania Adventures wageni wetu kabla ya kupanda mlima huwa wanapanda mti," alisisitiza Zainab.

Afisa Mhifadhi Mkuu wa KINAPA, Gladys Ng'ambi, alisema kuwa kwa mwaka huu wameongeza lango  lango la Machame na Lomosho kwa ajili ya maadhimisho hayo ambayo miaka ya nyuma lilikuwa likitumika lango la Marangu pekee.

Aidha alisema kuwa zoezi la kupanda mlima kwa ajili ya sherehe za uhuru litatanguliwa na zoezi la kufanya usafi wa mazingira ndani ya hifadhi hiyo.


Juhudi za pamoja kati ya ofisi ya  Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, kampuni ya ZARA Adventure, na wadau wengine katika kuboresha utalii na kuhifadhi mazingira ya Mlima Kilimanjaro zinathibitisha dhamira ya dhati ya kulinda hazina hii ya asili kwa vizazi vya sasa na vijavyo.








0 Comments:

Post a Comment