RAIS SAMIA MGENI RASMI MKUTANO WA BAWACHA




MWENYEKITI wa Taifa wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA),  Freeman Mbowe amesema Rais  Samia Suluhu Hassan ameridhia kuwa mgeni rasmi katika mkutano wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ulioandaliwa na Baraza la Wanawake la chama hicho  (Bawacha).


Mkutano huo wa BAWACHA unatarajiwa kufanyika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro  Machi 8, 2023 ambapo Mbowe amesema na yeye atakuwa kwa ajili ya kumpokea.


Akizungumza na waandishi wa habari leo, Machi 5, 2023 jijini Arusha, Mbowe amesema kuridhia kwa Rais Samia kumetokana na mazungumzo waliyofanya na Rais, Samia baada ya kukutana kwenye ikulu ndogo ya Arushasiku chache zilizopita.

“Nikitambua namna ambavyo tumefanya kazi na Rais Samia tumekubali tumualike naye amekubali kuhudhuria aje awasikie wakinamama wa Chadema, kina mama wa upinzani," amesema Mbowe na kuongeza.


.....Siku zote anawasikiliza wakina mama wa chama chake, aje awaone atambue kazi kubwa inayofanywa na akina mama wa Chadema kwa hiyo Rais atakuwa mgeni rasmi katika tukio letu na mimi nitakuwepo kumpokea,”.


Mbowe amesema katika mkutano huo pia wamealika wanawake washuhuri kwenye maeneo mengine mbali na siasa pamoja na wale  itikadi mbalimbali za kisiasa huku akisisitiza kuwa maadhimisho hayo si ya Chadema bali ya wanawake wote duniani.


Machi 8, kila mwaka ni siku ya kinataifa ya Wanawake ambapo wanawake hukutana kujadiliana kuhusu mafanikio na changamoto walizopitia katika sekta mbalimbali na namna ya kukabiliana nazo.

Kauli mbiu ya siku ya wanawake mwaka 2023 ni "Dijitali; Uvumbuzi na Teknolojia kwa usawa wa Jinsia.".

Kwa kauli mbiu hii tunaona umuhimu wa wanawake kushiriki katika  masuala ya teknolojia na uvumbuzi ili kuwawezesha kuendelea kutimiza ndoto zao katika nyanja mbalimbali.

Matukio mengi yameripotiwa juu ya wanawake kukumbwa na unyanyaji katika sehemu za kazi, biashara, kwenye ndoa na hata kwenye mitandao ya kijamii .

Hivyo ni wakati sasa kwa jamii kuamka na kuungana kwa pamoja kuhakikisha mwanamke na mtoto wa kike wanapata haki zao ikiwemo kupewa fursa za elimu, ajira, uongozi na kuheshimiwa  sawa wa wanaume .






0 Comments:

Post a Comment