Vijiji Vya Ngorongoro Vyarejeshwa Kwenye Orodha, Kufanya na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa


Serikali ya Tanzania imerudisha vijiji vya tarafa ya Ngorongoro pamoja na maeneo mengine yaliyokuwa yameondolewa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura. 




Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, ametangaza kuwa vijiji 12,333, mitaa 4,269, na vitongoji 64,274 vitashiriki uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.





Akizungumza jijini Arusha tarehe 16 Septemba 2024, Mchengerwa alisema, “Matangazo haya yanajumuisha maeneo yaliyokuwa yamefutwa awali kwa mujibu wa Tangazo la Serikali namba 673 na 674, ambayo yalihusisha pia Tarafa ya Ngorongoro. 


Lengo la hatua hii ni kuhakikisha kuwa maeneo haya yanapata uwakilishi mzuri kiutawala pamoja na huduma za kijamii na kiuchumi zinazowiana na mahitaji ya wananchi.”


Mchengerwa alisisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye uchaguzi huo na kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura kwa mustakabali wa maendeleo na kuendeleza juhudi za serikali katika kujitafutia maendeleo endelevu. 


Alisema, “Tunahitaji kila mwananchi kushiriki katika kuunda serikali ya wananchi kidemokrasia.”



Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Mohamed Bayo, alipokea kwa furaha tamko la serikali la kurejesha vijiji 65 na vitongoji 242 vilivyokuwa vimefutwa, akisema, “Tumepokea kwa furaha sana tamko la Serikali kurejesha vijiji 65 na vitongoji 242 vilivyokuwa vimefutwa. 


Hii itasaidia katika kuweka uwakilishi mzuri wa wananchi katika uchaguzi.”



Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Musa Miseile, alitaka viongozi wa mkoa kuhakikisha kuwa uchaguzi unakuwa huru na wa haki bila kuonesha upendeleo wowote wa vyama vya siasa.



Awalu Hali ya Ngorongoro ilikuwa tete, hivyo kupekea kufanyika maandamano ya yaliyowahusisha wenyeji wa eneo hilo ambao ni jamii ya kifugaji ya Wamaasai yaliyofanyika mnamo Agosti 18, 2024. 



Maandamano hayo, yaliyoshirikisha wanaume, wanawake, na vijana wa kabila la Wamasai, yalipinga kunyimwa huduma za msingi, ubaguzi, na haki yao ya kuishi katika ardhi ya Ngorongoro. 



Waandamanaji walibeba mabango na walifunga barabara yenye shughuli nyingi ya Ngorongoro-Serengeti.


Maandamano haya yalijiri wakati ambapo serikali inatekeleza mpango wa kuwahamisha Wamasai zaidi ya 110,000 kutoka Ngorongoro kwenda maeneo mengine kama Msomera, Sauni, na Kitwai, umbali wa zaidi ya kilomita 300 kutoka makazi yao ya sasa. 


Serikali inaeleza kuwa uhamisho huu ni muhimu kwa ajili ya kuhifadhi Eneo la Hifadhi la Ngorongoro, ambalo ni sehemu ya Urithi wa Dunia wa UNESCO.


Rais Samia Aihakikishia Ngorongoro Uchaguzi Kuendelea Kama Ulivyopangwa

Ingawa serikali inasisitiza kuwa uhamisho ni hiari, Waziri wa Maliasili na Utalii na msemaji wa serikali walieleza kuwa serikali ina mpango wa kuja na sheria itakayoondoa hali ya sasa inayoruhusu makazi ya watu ndani ya Ngorongoro.


 Ili kuvutia wakazi kuhama kwa hiari, serikali imeendelea kujenga nyumba bure kwa wahamiaji na kutoa usafiri wa kutoka Ngorongoro hadi Msomera. 


Hadi Aprili 2024, serikali iliripoti kutumia Shilingi bilioni 286 katika juhudi za uhamisho huo, ambapo takriban wakazi 8,364 wamehamishwa tangu Julai 2022.


Miongoni mwa madai ya Wamasai wengi waliobaki Ngorongoro wanailalamikia serikali kwa vitendo vya kibaguzi, ikiwemo mahitaji ya vibali maalum vya kuingia na kutoka Ngorongoro. 


Wakazi pia wamelalamikia kuondolewa kwa huduma muhimu kama vile elimu na afya, huku fedha zikielekezwa Msomera. 


Mbunge wa Ngorongoro na mashirika ya haki za binadamu wameripoti kuwa sehemu kubwa ya fedha za maendeleo na huduma za jamii zimeendelea kuondolewa Ngorongoro.


Wakazi wa Ngorongoro wanalalamikia pia kunyimwa haki yao ya kupiga kura. 


Tarehe 3 Agosti 2024, viongozi na wakazi wa Ngorongoro walidai kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imehamisha majina ya wapiga kura kutoka Ngorongoro kwenda Msomera, ambapo asilimia 2 tu ya wakazi wa Ngorongoro wamehamia. 


James Moringe Mollel, Diwani wa Loitile, alisema, “Tumeshangaa na kusikitishwa kwamba Tarafa nzima ya Ngorongoro ambayo imebaki na wakazi 110,000 hatutapiga kura kwenye vituo vyetu.”




Hali hii inatakiwa kufuatiliwa kwa karibu, kwani inahusu haki za msingi za wananchi na usawa katika upatikanaji wa huduma na haki ya kupiga kura.

0 Comments:

Post a Comment