KAMATI YA BUNGE YAKOSHWA NA UJEZI WA BARABARA KUELEKEA KRETA YA NGORONGOROSHWA



KAMATI ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeshauri teknolojia iliyotumika kujenga barabara kutoka geti la Seneto hadi Kreta ya Ngorongoro yenye urefu wa Kilomita 4.2 itumike kwenye hifadhi nyingine nchini.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa kamati, Timotheo Mzava, leo Machi 15,2023 wakati kamati hiyo ilipofanya ziara ya kukagua miundombinu ya barabara  ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Amesema kuwa kamati yake imefarijika na uamuzi wa kujenga barabara hiyo na kuipongeza Serikali kwa kutoa fedha ya ujenzi huo.


"Tunaipongeza Wizara na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kusimamia vizuri ujenzi wa barabara hii, miaka ya nyuma tulipotembelea huku ilikuwa ni shida kubwa kwa watalii lakini baada kukamilika (barabara) tumeshuhudia ubora wa  huduma kwa wageni wanaoelekea bonde la Kreta umeimarika na malalamiko yamepungua," amesema Mzava.

Ameishauri Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kuendelea  kuboresha barabara zote za kuingia ndani ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ili ziwe bora na kuendelea kupitika  muda wote wa mwaka.

‘’Kwa kuwa teknolojia hii ni nzuri na rafiki kwa mazingira hasa kwa maeneo ya Hifadhi kamati inashauri  teknolojia hii iendelee kutumika maeneo mengine yenye hifadhi ndani ya nchi yetu," amesisitiza Mwenyekiti huyo wa kamati Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii.


Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,  Mary Masanja amesema kuwa Serikali itaendelea kutekeleza ushauri wa kamati ya Bunge kuboresha miundombinu ya barabara hasa za mawe ambazo ujenzi wake ni nafuu kulinganisha na barabara ya lami.

"Barabara hii ina urefu wa  kilometa 4.2, bajeti yake ilikuwa shilingi  1.9  Bilioni lakini tukajenga kwa shilingi 1.7 bilioni hivyo  kuokoa kiasi cha shilingi 200 milioni, tutaendelea kutumia teknolojia hii katika maeneo yetu ya hifadhi hasa yenye barabara korofi," amesema Masanja. 

Amesema kuwa wanamshukuru Rais,  Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za ujenzi wa miundombinu ambayo ni sehemu mkakati wa kufikia  watalii Milioni 5 ifikapo mwaka 2025 na kuongeza fedha za kigeni kutoka asilimia 17.5 hadi zaidi ya 30 kwa miaka ijayo.

0 Comments:

Post a Comment