MAHAKAMA YAWANOA WATUMISHI WAKE KUTUMIA MFUMO MPYA WA KIELEKTRONIKI

MAHAKAMA ya Tanzania imetoa mafunzo kwa viongozi na watendaji wake juu ya namna ya ya kutumia ya mfumo wa kielektroniki wa kuratibu mashauri , (E-CMS), unaolenga kuongeza ufanisi wa kazi katika kutoa na kupata huduma za mahakama kwa urahisi.

 

Aidha, mfumo huo wa kieleketroniki utawezesha mahakama kuondokana na majalada ya makarasi kwani kila kitu kitapatikana kwa njia ya kielektroni ikiwemo kumbukumbu za kesi kuanzia

ufunguaji , usikilizwaji na utoaji wa taarifa za mashauri hayo.

 

 

Mafunzo hayo yamefanyika leo Jumamosi Machi 18, 2023 katika Kituo Jumuishi cha utoaji haki, Arusha yakiwashirikisha Manaibu Wasajili, Wakurugenzi,  wakurugenzi wasaidizi, Mahakimu wakazi wafawidhi ngazi zote, viongozi na maofisa Tehama wa  Mahakama zote nchini ambao watakuwa na jukumu la kwenda kuwafundisha wenzao kwenye maeneo yao ya kazi .

 

 




Akifungua mafunzo hayo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Jaji, Joachim Tiganga, amesema kuwa  mfumo wa E-CMS sio tena kwa ajili ya makarani pekee kama ilivyokuwa kwenye mfumo wa awali  bali unakwenda kutumika kwa asilimia 100 kwa majaji na mahakimu.

 

 

Hata hivyo amesema kuwa mifumo mizuri ni jambo moja na kuitumia ipasavyo ni jambo lingine hivyo akaonya kuwa endapo walengwa wataacha kuitumia  katika kutatua matatizo au kurahisisha utendaji kazi wao basi  mifumo hiyo ni sawa na kuwa haipo.

 

Jaji Mfawidhi, Tiganga amesema kuwa mahakama imekuwa na safari ndefu ya maboresho iliyoanza   mwaka 2014 kwa kutumia TEHAMA  (JSDS toleo la kwanza) na mwaka  2018 walihamia kwenye toleo la pili ambapo walikuwa wakisajili mashauri kwa njia ya kielektroniki (e-filing) na kufanya malipo kwa njia ya kielektroniki (e-payment) ambapo haya ya sasa ni awamu ya tatu.

 

Maboresho haya yamelenga kufikia malengo ya serikali na ya Mahakama ya Tanzania  ambapo mifumo hiyo ya maboresho imekuwa ikijengwa na wataalam wa ndani jambo alilosema kuwa ni la kujivunia kwani hata watu kutoka mataifa mengine ya Afrika wamekuwa wakija kujifunza.

 



“Kwa mfumo huu tunaoenda kuuanza utawashirikisha zaidi ninyi mahakimu na majaji kuliko makarani kama ilivyokuwa kwenye mifumo iliyotangulia si kwamba makarani watakuwa hawana ‘roll’ hapana bali yale mengi waliyokuwa wakifanya sasa yanaenda kufanywa na ninyi (mahakimu na majaji),” alisisitiza jaji Tiganga.


 

Hata hivyo majaji hawakushiriki mafunzo hayo ambapo alisema kuwa anataarifa kuwa wanatarajiwa kuandaliwa mafunzo mwenzi Aprili ingawa washirki hao walielekezwa kwa hatua za awali wakawafundishe.

 

“Uwepo wa mifumo hautuhakikishi kuwa tutakuwa bora bali tutakapoenda kuitumia mifumo hiyo kutatua matatizo yetu na kurahisisha utendaji wetu wa kila siku. Malengo ya mifumo hii ni kuwafikia wananchi, tupo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi,” amesema jaji Tiganga na kuongeza.

 

 

… Malengo ya mifumo hii  tunataka tuwaridhishe  wananchi walau kwa asilimia 80 kwa kutumia TEHAMA ni matarajio yetu wote kuwa mtaondoka hapa mkiwa watu bora sana na ujuzi mtakaopata muende mkawafundishe wenzenu vizuri na wao waweze kuutumia,”.

 

 

 


 

Jaji Mfawidhi huyo wa Makahama Kuu Kanda ya Arusha, amesema kuwa mahakama kwa kutumia wataalam wake wa ndani imejenga mifumo huo wa kielektroniki utakayotumika kuratibu shughuli zote za kimahakama na za kiutawala.

 

“Mifumo hii itarahisisha sana upatikanaji wa taarifa mbalimbali za utendaji wa Mahakama kwa usahihi na kwa wakati, taarifa hizi zinakweza kusaidia kwenye upangaji wa rasilimali watu, usimamizi wa shughuli za kimahakama pamoja na kufanya maamuzi ya haraka pale itakapotakiwa,” amesisitiza Jaji Tiganga.



 

Akiongea na washiriki hao, Mkurugenzi wa Menejimenti ya mashauri, Mahakama ya Tanzania, Desderi Kamugisha, amesema mfumo huo wa kidigitali utawezesha shughuli zote za usikilizaji wa mashauri kufanyika  kielektroni kuanzia uchukuaji wa mwenendo wa ushahidi  mpaka hukumu vyote vitakuwa vinafanyika kwenye mfumo.

 

“Mfumo huu (E-CMS) utakuja kuunganishwa na mfumo wetu mpya tunaotaka kuanza kuutumia muda sio mrefu wa uchukuaji wa mwenendo na utafsiri wa mwenendo wa mashauri… ambapo jaji akiwa mahakamani haitaji tena kuandika,” alisema Kamugisha na kuongeza.

 

…Jaji anasikiliza tu kwani mfumo wenyewe ndiyo unachukua sauti na unaibadili ile sauti kuwa katika maandishi na kuwa nakala laini (soft copy) na itaingia kwenye jalada la kielektroniki la mfumo wa mashauri  hivyo kila kitu kitaenda kwa njia ya mtandao na tutaachana na njia za kawaida (makaratasi) za usikilizaji wa mashauri,”

 

 

Kamugisha amesema mfumo E-CMS wa kuratibu shughuli za mashauri kwa njia ya kielektroniki kuanzia hatua ya ufunguaji na kuwa baada ya kuanza kutumika hawataruhusu tena ufunguaji wa mashauri kwa njia ya kawaida.

 

“Watu wote wenye mashauri mahakamani wakiwemo Ofisi ya  Taifa ya mashitaka, mawakili wa kujitegemea na wananchi anaweza kufungua kwa njia ya mtandao kwa kupitia mfumo huo,”amesema Kamugisha na kuongeza.

 

…Baada ya hapo shauri hilo litaenda kwa afisa wa mahakama katika ngazi husika kwa ajili ya kulisajili, likishasajiliwa kimfumo litaenda kwa hakimu au jaji  kwa sababu mfumo  unapanga wenyewe kwa kuangalia jaji au hakimu ana mashauri mangapi,”.

 

“Baada ya hapo tutakuwa na jalada la kielektroniki ambalo hapo tutakuwa tumeondokana na majalada ya mahakama yale ya makaratasi. Shughuli zote za usikilizaji wa mashauri utakuwa wa kielektroni kuanzia uchukuaji wa mwenendo wa ushahidi  mpaka hukumu vyote vitakuwa vinafanyika kwenye mfumo,” .

 

“Kwa hiyo kumbukumbu zote za shughuli za mahakama zitafanyika kwenye mfumo hivyo mwenye shauri kama ni wakili au mwananchi alilifungua anaweza kuziona bila hata kufika mahakamani,”

 

Kamugisha alifafanua kuwa mfumo huo utakuwa unatoa taarifa za mashauri hivyo kimsingi mfumo huo umelenga kuondokana na matumizi ya karatasi katika shughuli za mahakama kuanzia ufunguaji , usikilizwaji na utoaji wa taarifa za mashauri hayo.

 

 


 

Kwa upande wake, Msajili Mkuu wa Mahakama, Wilbard Chuma, amesema mahakama mtandao itaongeza ufanisi wa kazi, kutoa na kupata huduma za mahakama kwa urahisi ambapo hatua hiyo  ya mafunzo ya leo yanawafikisha karibu na mwisho wa safari wa kuwa mahakama mtandao ambapo shughuli zake zote zitafanyika kidigitali.

 

"Safari ya ujenzi wa matumizi ya mfumo ni ndefu, wataalam wa ndani wamekamilisha kazi kubwa tunaenda kupitishwa katika mfumo na yapo mabadiliko makubwa yamefanyika katika mfumo ikiwemo moduli mpya ya mashauri ya familia," amesema Chuma.

 


Amesema kuwa mpaka wanafikia kufungua mafunzo hayo kazi haikuwa  rahisi kwani  wataalam wao  wa TEHAMA wamefanya kazi kubwa ya kujenga mfumo na kufanyia maboresho kwa kuwatumia majaji wa mahakama ya rufani na wale wa mahakama kuu.

 

Chuma mesema kuwa ilionekana kuna umuhimu wa kuwafundisha wakufunzi ambao wataenda kufundisha wengine walioko huko kwenye mahakama zote nchini ili kuhakikisha mifumo hiyo inatumika kwa ufasaha na ufanisi zaidi

 

Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania na Programu ya Uboreshaji wa Huduma  awamu ya pili wa mwaka 2020 mpaka 2025, unalenga kuboresha ufanisi na uwazi wa upatikanaji wa haki kwa wananchi kwa urahisi zaidi.

Awamu ya kwanza ya mpango huo  ulilenga  kuimarisha miundombinu na kusogeza huduma za utoaji haki karibu na wananchi ambapo  ulifanikisha uwepo wa  miundombinu ikiwemo ya majengo na  Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ,(TEHAMA), imeboreshwa ndani ya Mahakama, jambo lililowasaidia wananchi wengi kupata huduma za haki katika mazingira rahisi na kwa gharama nafuu. 

 

Mipango hiyo ya mahakama inatekelezwa na ufadhili wa mkopo wa Benki ya Dunia wenye masharti nafuu ikilenga kuboresha utoaji huduma za mahakama  ili kusaidia kupambana na umaskini pamoja na kudumisha usawa kijinsia .

 

 

.

0 Comments:

Post a Comment