KESI YA WANANCHI WA LOLIONDO KUSIKILIZWA MEI



KESI ya wananchi wa watano wa Loliondo  wanaopinga tangazo la Waziri wa Maliasili na Utalii lililotumika kuwaondoa kwenye maeneo yao  imepangwa kuendelea   Mei 4, 2023 baada ya upande wa jamhuri kuomba muda wa kuleta mapitio ya mwanasheria wa serikali kuhusu katazo hilo.

Shauri hilo la mapitio namba 21/2022 limekuja leo Machi 14,2023 mbele ya Jaji Mfawidhi, Joachim Tiganga wa mahakama Kuu Kanda ya Arusha kwa ajili ya kutajwa.

Wakili wa Serikali, Mkama Msalama akiwasilisha ombi hilo amesema kuwa muda huo utamwezesha kukaa na watu wa Wizara ya Maliasili na Utalii  ili kulipitia kwa undani  tangazo hilo huku akisisitiza kuwa watu hao  watapatikana muda wiki hii.

Mahakama hiyo iliridhia ombi hilo na kuwapa muda wa siku saba (mpaka Machi 21) upande wa Jamhuri kuleta mahakamani hapo kiapo kinzani cha maombi hayo ambapo upande wa waleta maombi watatakiwa kuwasilisha majibu yao ndani ya siku saba (mpaka Machi 28,2023)  endapo watahitaji kufanya hivyo  .

 Kwenye shauri hilo wananchi hao, Latang’amwaki Ndwati , Ndalamia Taiwap, Megwari Moko, Ezekile Sumare na Latajewo Sayari wanawakilishwa na mawakili,  Joseph Shangay, Denis Moses na Hamis Mayombo huku wajibu maombi Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri wa Maliasili na Utalii wakiwakilishwa na wakili wa Serikali,  Msalama.

 

 

Wananchi hao wa vijiji vilivyokuwa kwenye Tarafa ya  Loliondo waliofungua shauri hilo wanadai kuwa waliathirika na mchakato wa eneo hilo la Kilometa za Mraba 1,500  kutangazwa na serikali kuwa pori tengefu la Pololeti.

 

Wananchi hao wanaiomba  mahakama itoe zuio dhidi ya tangazo la serikali namba 421 la  Juni 17, 2022  kwa kuwa ni batili kwa kile wanachodai kuwa  halikufuata taratibu za kisheria hivyo si halali na halipaswi kutumika.

 

Katika ombi lao la pili wanaiomba mahakama itamke kwamba serikali,  taasisi na watu wake wasiruhusiwe kuingia kwenye eneo hilo kuendesha operesheni zao mpaka mahakama hiyo itakapotoa uamuzi wa maombi yao.

 

 

 

 

 

.

0 Comments:

Post a Comment