TUMECHOKA HABARI VIPORO- WASIOSIKIA



WATU wenye ulemavu wa kutosikia (Viziwi) wamesema wamechoka kupokea viporo vya habari ambapo wametaka serikali na vyombo vya habari kuweka wakalimani wa lugha za alama ili na wao wapate haki ya mawasiliano kama wanavyopata wananchi wengine.



Aidha wameitaka ofisi ya Waziri Mkuu kuonyesha mfano kwa kuanzisha bodi inayosimamia lugha ya alama kama ilivyo kwa bodi zingine.



Hayo yalisemwa leo Desemba mosi, 2022 na Mwenyekiti wa chama cha Viziwi nchini, ( CHAVITA), Selina Mlemba wakati akizungumzia maandalizi ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu duniani ambayo kitaifa yanafanyija jijini arusha.



Alisema kuwa vyombo vingi vya habari havina wakalimani wa lugha na hata wakiwa nao huwatumia kwenye vipindi vichache huku akidai walalimani hao huonyeshwa kwenye picha ndogo na rangi inayotumika haiwawezeshi wenye ulemvu kumuona.



"Karibu hotuba zote za viongozi wetu wa kitaifa hutolewa bila kuwapo mkalimani, mbaya zaidi mara chache tumekuwa tukipata viporo tena katika nyakati ambazo si sahihi," alisema Mlemba kwa masikitiko na kuongeza.



...Mfano mzuri mara nyingi hotuba za Rais hazihusishi wakalimani na hivyo kutupita kana kwamba Amiri Jeshi huyu mkuu wa Taifa si kiongozi wetu,".





Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Kanisa la Viziwi Tanzania,  Mchungaji, Joseph Hiza alisema wanajisikia vibaya wanapokosa hotuba za Rais pale anapohutumia Taifa au kuzindua miradi mbalimbali jambo alilosema kuwa walemavu wana haki ya kupata taarifa hiyo kama wananchi wengine. 



alisema kuwa matatizo ya walemavu hasa viziwi na wasioona ni ya kimawasiliano hivyo wamekuwa wakisahaulika kwenye mipanho, sera na utoaji huduma mbalimbali ikiwemo habari na elimu.




"Kutokana na changamoto ya mawasiliano walemavu wamejikita kwenye hatari hata ya kupata maambukizi ya magonjwa ya kuambukiza niliwahi kukutana na vijana niliosoma nao kule Njombe kule kuna jamii kubwa ya watu wenye ulemavu wa kusikia,"  alisema Hiza na kuongeza.


...Nilipoongea nao wengi wamepata maambikizi ya virusi vya UKIMWI baada ya kukosa elimu juu ya namna ya kujikinga ambapo walikuwa wakidanganyana kuwa ukila nyama ya nguruwe huwezi kupata maambukizi hayo hali iliyowapelekea wengi wao kuangamia,"



"Tunaomba wenye vyombo vya habari muongeze nguvu zaidi katika kuhakikisha inatekeleza sheria zinazozingatia mahitaji na haki za watu wenye ulemavu ikiwamo hii ya mawasiliano kwa kuhakikisha mmnaajiri  wakalimani kwa wingi kurekebisha mapungufu yaliopo,".


Akitoa mfano mwingine alisema kwa sasa kuna timu zinapita kila  Mkoa kihamasisha chanjo lakini viziwi wameendelea kuachwa katika hilo na hakuna mkakati wowote wa kujaribu kuwafundisha na hali hiyo imetokea pia kwa elimu ya magonjwa ya mlipuko  kama vile Ebola.


Aidha alisema ni hatari kwa nchi kwenda kinyume na mikataba ya kimataifa ambayo imeisaini na kwa msingi huo mara nyingi serikali inashindwa kupeleka ripoti katika mashirika ya kimataifa kwa sababu ya kuogopa kuumbuka kutokana na kutotekeleza  ipengele vingi vilivyoainishwa.


Kwa upande wake Katibu wa Shirikisho la Vyama vya wenye ulemavu nchini, Jonas Lubalo alisema kuwa ni vema mchakato wa kupatikana kamusi ya lugha ishara ulakamilika huku akitaka viongozi na waandishi wa habari kuzingatia makundi yote ya walemavu pindi wanapoandaa taarifa zao.


"Lazima tutafakari pamoja ili walemavu wote wapate haki ya habari. Kwa mfano walemavu wa akili ukimuandikia makala ndefu hawezi kuelewa au wale wasioona hawawezi kusoma gazeti," alisema Lubalo na kuongeza


... Walemavu wa kuona janga la KORONA liliwagusa zaidi kwani wakati wataalam wa afya wakisisitiza watu waepuke kugusana lakini wao hawawezi kuwasiliana bila kugusana,'.


Siku ya walemavu duniani huadhimishwa Desemba 3, ya kila mwaka ambapo mwaka huu kauli mbiu ni suluhisho la mabadiliko kwa maendeleo jumuishi. Nafasi ya ubunifu katika kuchangia dunia fikivu na yenye usawa.






0 Comments:

Post a Comment