WANANCHI KIA WAPINGA KUNYANG'ANYWA ARDHI YAO, RC AELEZA SABABU ZA KUTUMIA POLISI WENYE SILAHA


 

WANANCHI wa vijiji  vilivyo maeneo ya kuzunguka Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, (KIA), wamelalamikia hatua zinazochukuliwa na serikali za kuwanyang’anya  ardhi yao kupitia zoezi la uwekaji mipaka walilodai lilifanyika kibabe bila kuzingatia  sheria  huku likiwashirikisha polisi wengi wenye silaha za moto na magari ya maji ya kuwasha.

 

Aidha, wananchi hao wanapinga kuitwa wavamizi kwenye eneo hilo kwa kile walichodai kuwa mwaka 1969 aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati, Julius Kambarage Nyerere alifika hapo na kufanya kikao na wazee wao ambapo walikubali kumpa ardhi hekta 460 ambazo mpaka sasa hawajaziendeleza zote hivyo si sawa kuwaita wavamizi.

 

Pia wamelalamika zoezi hilo kutokuwa shirikishi kwani wataalam wa uthamini walioambatana na polisi wakifika kwenye maeneo yao na kuwaamrisha  wasimame mbele ya nyumba wanawapiga picha, wanahesabu miti na makaburi kisha wanawapa barua ya kuwasilisha malalamiko kwa mtu ambaye hawamjui.

 

Wananchi hao wameyasema hayo kwa nyakati tofauti Novemba 25, 2022 wakati wakifanya mahojiano na wandishi wa habari waliowatembelea kwenye makazi yao.


Waandishi wa habari walishuhudia gari la polisi likiwa na polisi wenye silaha na gari la maji ya kuwasha vikiwa vimeegeshwa pembeni ya barabara kwenye kijiji cha Tindigani kata ya Kia.

 

Mzee, Moses OleMunga mkazi wa Kijiji cha Tindigani alilalamika kuwa , Serikali inawaondoa kwenye  kwenye ardhi yao ya  asili kwa lazima na haiwaelezi inawapeleka wapi jambo alilodai kuwa wamekuwa kama watoto yatima ndani ya Taifa lao.

 


“Mimi nina miaka 64 nimezaliwa hapa sijui serikali inatufikiriaje,  inatunyang'anya mashamba yote tunayolima tunayolishia watoto. Wanasema sisi tumevamia uwanja wa ndege (KIA) wakati uwanja wa ndege umeanza kujengwa sisi tuko hapa ni vijana wadogo tunauona, “ alisema OleMunga na kuongeza.

 

…Hatuelewi utaratibu wao hawataki hata kutusikiliza inashangaza sana. Mwanzo Mwalimu Nyerere alizungumza na wazee wetu wakampa hekta 460  hawajamaliza kuzitumia sasa wanatunyang'anya hizi nyingine..Hakuna nchi yenye uwanja wa ndege wenye eneo kubwa kama hili,”.. 

 

“Hapa tumeshaongea na viongozi wengi (Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman) Kinana wakati akiwa akiwa katibu mkuu wa CCM, Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa wanatusikiliza na mara zote wamekuwa wakituambia watatuletea majibu lakini  hawajarudi tena,”.

 

“Mimi sihitaji fedha haiwezi kunisaidia,  mimi nahitaji mashamba yangu yananisaidia kutunza familia.Mimi nimezaliwa hapa, nimekulia hapa, nikaoa nikiwa hapa, nikapata watoto na mke wangu mkubwa akafariki nikaoa mwingine naishi naye sasa hivi naye amezeeka kama. sijui tunavyoondolewa hapa sijui naenda naye wapi kuaza maisha sijui tutaanza maisha kinamna gani,”.

 


Mwananchi mwingine wa kijiji cha Chemka kata ya Masama Tundugai,  Aziza Juma alisema kuwa yeye ni mzaliwa wa eneo hilo na amezaliwa kabla ya uwanja wa KIA haujajengwa hivyo anashangaa kusikia akiwambiwa kuwa waondoke aneo hilo kwa madai kuwa ni wavamizi.

 

“Nimeshangaa juzi watu wamekuja kunivamia wakiwa na magari ya polisi tena bila taarifa kidogo niangushwe na presha nikaambiwa niondoke hapa ni eneo la KADCO (Kampuni ya uendelezaji uwanja wa KIA) . Sisi tukija hapa tulikuta ni pori ni shida kubwa nashangaa sasa naambiwa hili ni eneo la KADCO lakini najiuliza uwanja mbona uko mbali sana na sisi,” alisema Aziza huku akilia kwa uchungu na kuongeza.

 

…Wamekuja wameandika namba kwenye mlango wakatuhesabu pamoja na watoto wangu  wakahesabu miti, migomba na makaburi wamekuta hapa makaburi karibu 40 wanasema ardhi ni ya serikali hivyo hawawezi kutupa fidia ya ardhi,”. 

 


“Wakati KIA imeanza kujengwa mimi nilikuwa naiona nilikuwa na umri mdogo. Nilikuwa  nachuma mchicha naenda kuuza kule wakajenga wakamaliza wakapanda ile mijohoro wakasema mwisho wa KIA utakuwa hapo baadaye wakasema mwisho wa KIA utakuwa barabara ya Naiberera sasa wanasema inakuja mpaka huku Chemka.”  Alisema, Esther Thomas (67), mwanakijiji wa Chemka.

 

…Sasa KIA iko mbali zaidi ya kilometa 15 kutoka hapa eneo hilo lote mpaka uje uingie huku mashambani unajiuliza watakuja kuegesha ndege?. Sisi tumeshangaa hapa juzi tumevamiwa na askari karibu 40 na magari zaidi ya nane hatukupewa nafasi ya kusikilizwa unaambiwa sema hivi mimi sikuweza nilishikwa na presha nikashindwa,” 

 

“Serikali ituambie kwa nini tunavamiwa kwenye kijiji chetu cha Chemka hatuko kata ya KIA tuko kata ya Rundugai. Sasa tunashangaa wanaunganisha na kata ya Kia. Mimi na familia yangu tunamiliki ekari 40 ambazo tnazitumia kwa makazi na kilimo,”.

 

“Serikali ni watu na sisi ni watu. Serikali waingie katikati wajue watafanyaje , waelewe hatutaki fidia ya hela hayo makaratasi sisi tunapeleka wapi? Wao wabaki na eneo lao na sisi tubaki na maeneo yetu ambayo ni haki yetu.”. 

 

Mwandishi wa habari hizi  alimtafuta wakili, Moses ambaye alitolea ufafanuzi wa kisheria juu ya  taratibu zinazopaswa kufuatwa endapo serikali inahitaji ardhi kwa ajili ya lengo mahsusi sana  ambapo alisema  sheria ya ardhi sura ya 113 na  ya ardhi ya  vijiji na sheria ya utwaaji wa ardhi sura ya 118 zote zinatoa muongozo huku sikisisitiza kuwa  kila mtu anahaki ya kukalia ardhi bila kubughudhiwa na mtu yeyote.

 

“ Ikitokea kuna haja kwa lengo mahsusi sana ardhi inatakiwa kuchukuliwa kuna taratibu za kufuatwa. Sheria imeweka bayana kuwa itabidi kuwa na mazungumzo ili watu walipwe fidia kwa kupewa ardhi mbadala lakini imesisitiza utawaondoa watu  ikiwa kuna jambo mahsusi linalokulazimu kuichukua ardhi hiyo," alisema wakili Moses na kuongeza.

 

... Inatakiwa afike mthamini kuithaminisha ardhi hiyo, lazima wananchi wanaoishi kwenye hiyo ardhi washirilishwe wanaporidhia ndipo mchakato huo unaweza kuendeleza,".

 

 Alisema kuwa uthamini huo unajumuisha ardhi na maendelezo mengine yaliyofanyika kwenye ardhi hiyo na kwani watu  wengine wanalinda ardhi kwa kuwa inalinda imani za mila zao na endapo wananchi hawajaridhika wanaweza kwenda mahakamani kupinga uchukuaji wa ardhi na kwa hatua ya awali wanaweka zuio kuzuia zoezi hilo.

 

Alifafanua kuwa endapo zoezi la udhamini litafanyika kwa kutumia polisi wenye silaha ile dhana na ushirikishaji inakuwa haipo kwani zoezi hilo linakuwa limefanyika kwa kutumia nguvu hivyo huo unakuwa ni uporaji.

 

Akijibu hoja hizo za wananchi,   Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu alisema kuwa uwanja huo ni mali ya serikali na una hati ya miaka 99 ambapo kutokana na kutoendelezwa kwa muda mrefu kuna wananchi waliingia kwenye eneo hilo kwa kujua au kutojua.

 

Alisema kuwa  wameamua  kuweka mipaka kwa mujibu wa sheria kulingana na hati iliyopo na wameshamaliza zoezi hilo kwa upande wa Kilimanjaro na Arusha ambapo kwa sasa zoezi linaloendelea ni la  tathmini.

 

Babu alisema kuwa wananchi hao walishirikishwa na wakati akiapishwa kuwa mkuu wa mkoa Kilimanjaro,  mbunge wa jimbo la Hai, Saashisha Mafue  alikuwa akifanya kikao na wananchi hao aliwaeleza suala la uwekaji mipaka hivyo wananchi amefanya vikao sita na wananchi, viongozi wa kijiji na viongozi wa mila malaigwanan.

 

"Mimi mwenyewe nilifika pale nikafanya mkutano mkubwa na wananchi na viongozi nikatoa msimamo wa serikali na tukaelewana na nikawapa tarehe ya kuweka mipaka,” alisema Mkuu wa mkoa huyo na kuongeza

 

…Kwamba wanafanyiwa tathmini ya nyumba, migomba na makaburi ni sawa kwa sababu ardhi ile ni ya serikali na ina hati ya miaka 99.Kinachofanyika ni huruma ya Rais kwa wananchi wake kuwa wale waliovamia basi tuwape chochote wasiende kuhangaika,”.

 

RC Babu alisema kuwa mambo mengine yanaweza kuja endapo viongozi wa juu  wataangalia kuwa walikuwa watu hao walikuwa hapo muda mrefu walikuwa wanalima lakini kwa sasa utaratibu ndiyo huo huku akiwataka wananchi watoe ushirikiano.

 

 

“Baada ya kuzindua bikoni ya kwanza mimi nimeenda Rombo kukagua ujenzi wa madarasa huku nyuma wamevunja magari ya serikali vioo, wamempiga DC, wamempiga mwenyekiti wao wa kijiji na watu wengine,” alisema RC Babu wakati akifafanua ni kwa nini zoezi hilo lilifanyika chini ya ulinzi mkali wa polisi na kuongeza

 

…Wanataka kuichezea serikali sisi watupige tuwaache tu?  yaani wananchi mtupige viongozi wa serikali sisi tuwatizame tu?  kwa hiyo ndiyo maana mimi nimeongeza askari,".

 

 

Mkazi mwingine wa kata Tindigani ambaye hakupenda jina lake iandikwe gazetini kwa kile alichodai kuwa hali ya usalama kwenye eneo hilo ni mdogo alidai kuwa yeye amezaliwa kwenye eneo hilo  mwaka 1960 kabla ya uhuru na kabla ya uwanja wa KIA na kuwa eneo hilo walilirithi kutoka kwa mababu zao hivyo si sahihi kuitwa wavamizi wakati wao ndiyo walikuwa kwenye eneo hilo kabla ya KIA kuanzishwa mwaka 1969.


Awali mwanzoni mwezi Novemba wananchi wa vijiji hivyo walikutana kwenye kijiji cha Tindigani na kutoa tamko la kupinga kuondolewa kwenye eneo hilo.

 

 


Walidai kuwa babu zao walikuwa hapo kwa karne nyingi huku wakidai kuwa Wamisionari wa kwanza waliouona hata kudai wameugundua mlima Kilimanjaro, Dkt Ludwing Kraft na mchungaji, John Rebman wanasadikika kuwa ndiyo wazungu wa awali kuwaona wamasai kwenye eneo hili, mwaka 1840.

 


Wanadai eneo hilo ambalo limeitwa Kia baada ya Kata ya Masama Rundugai kugawanywa ndiyo chimbuko la Maasai huku wakirejea utafiti wa Profesa Issa Shivji wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam  alioufanya waka 1998 aliandika," Wamaasai wanaamini kwamba Naiterukop (mama) ambaye ndiye mwanzilishi wa jamii ya Maasai alitokea hapa,"

 


Wanadaiwa noti ya shilingi 100 ya mwaka 1960 na mwanzoni mwa miaka ya 1970 ilikuwa na picha ya Maasai,  picha hiyo inadaiwa ilipigwa katika eneo hili kabla ya KIA.

 

 

 

Pia Mwaka 1975 vijiji vitano vilisajiliwa kwenye eneo hilo chini ya sheria ya vijiji vya ujamaa ambavyo ni Sanya Station, Mtakuja, Majengo, Malula na Samaria.

 


Hata hivyo sheria ya serikali za mitaa namba 7/1982 ilifuta sheria ya vijii vya ujamaa ambapo kwenye eneo hilo vilisajiliwa vijiji viwili vya Tindigani na Chemka.

 

Agosti 1, 1985 Wizara ya Ardhi ilijenga kilometa za mraba 110 kwa kile ilichoeleza ni kuendeleza uwanja huo bila kuwashirikisha wananchi wanaoishi maeneo hayo jambo walilodai kuwa ni kinyume cha sheria ya unyakuaji ardhi ya namba 47 ya mwaka 1967.

 

Mwaka 1986 KIA ilipima eneo hili Farm No 1 Plan E5 255/18 ilisajiliwa kwa siri ikiwa na namba 23164 mwaka 1989.

 


Inadaiwa kuwa baada ya kubaini Wizara ya ardhi imeipa KIA hati hiyo kinyume na sheria wananchi walichukua hatua mbalimbali ikiwemo aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Freeman Mbowe kulizungumzia bungeni Novemba 10, 2003.

 

Pia kuna muhtasari wa kikao cha pamoja cha vijiji hivyo na KADCO  uliofanyika Machi 28, 2006 ambapo muhtasari huo unaeleza bayana kuwa kulikuwa na mgogoro wa ardhi baina ya pande hizo mbili.

 


Walidai kuwa licha ya mgogoro huo kufika bungeni mara kadhaa kati ya mwaka  2000 na 2006, KIA walipewa cheti cha ardhi na 22270 Aprili 20, 2006 kwa miaka 99.

 

 


0 Comments:

Post a Comment