UNWTO YAIPONGEZA TANZANIA, KUFANYA MKUTANO WAKE ARUSHA OKTOBA

 



SHIRIKA la Utalii Duniani, (UNWTO) limeipongeza Tanzania kwa kutengeneza mazingira yaliyowezesha kuvutia idadi kubwa ya watalii kuitembelea mara baada ya janga la UVIKO 19 hivyo kwenye uchaguzi ujao wa taasisi hiyo watapendelea ipate kiti kwenye kamati zilizopo ili waweze kubadilishana uzoefu.


Aidha Tanzania inatazamiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa 65 wa UNWTO  Kamisheni ya Kanda ya Afrika, (CAF), unaotarajia kufunguliwa rasmi na Rais, Samia Suluhu Hassan Oktoba 5, mwaka huu jijini Arusha ambapo washiriki ni pamoja na mawaziri wanaouhusika na masuala ya utalii kutoka nchi wanachama.




Hayo yamesemwa kwa nyakati tofauti leo Julai 7,2022 jijini Arusha na Mkurugenzi wa UNWTO ukanda wa Afrika, Elcia Grandcourt na Waziri wa Maliasili na Utalii, Pindi Chana wakati wa mkutano wa pamoja kati yao na sekretarieti ya UNWTO inayoandaa mkutano huo wa siku mbili unaotazamiwa kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 300.

 
Grandcourt ameelezea kuridhishwa na hatua zinazochukuliwa na Tanzania  katika kuweka tahadhari ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya UVIKO 19 ambapo alisema inabidi mataifa mengine yajifunze kutoka hapa.

"Tutapendekeza Tanzania na tutaiambia  dunia kuwa kuna mataifa kwa ukanda wa Afrika wanaotekeleza vizuri mpango wa kuchukua tahadhari kujilinda na kuzuia kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya UVIKO 19," amesema Mkurugenzi huyo wa UNWTO ukanda wa Afrika na kuongeza.

...Tumeangalia hoteli nyingi tumefurahishwa na vifaa walivyoweka na hatua za kiafya walizochukua kuhakikisha watu wanakuwa salama naamini hii inatuhakikishia usalama pia kwenye mkutano wetu wa Oktoba,".

Amesema kuwa kwa hayo aliyoyaona anatazamia kwenye uchaguzi ujao Tanzania ipate kiti kwenye halamshauri kuu UNWTO na pia kwenye kamati nyingine ili waweze  kushauri kwenye masuala ya utalii na yale ya maliasili 

Grandcout amesema maeneo mengine ambayo Tanzania itabadilishana uzoefu ni kwenye kamati  zinazoshughulika na masuala maendeleo endelevu, ushindani wa maeneo ya vivutio vya utalii, takwimu za elimu na  kujengea uwezo 


Grandcourt amesema kuwa hatua ya Rais Samia  kutangaza utalii wa Tanzania kupitia The royal Tour umeiweka vizuri Tanzania kwenye soko la  utalii kimataifa.

Akizungumzia hali ilivyo kwenye sekta ya utalii baada ya janga na UVIKO 19, Grandcourt amesema utalii umeanza kufunguka kwani hata walipokuja Arusha wameona kuna baadhi ya maeneo wameshindwa kuangalia hata vyumba vya hoteli kwani vimejaa wageni jambo alilodai kuwa linatia moyo si tu kwa Tanzania bali kwa bara zima la Afrika.


"Inatia moyo kuona wakati tumekuja hapa tulitua Arusha ndege ikiwa imejaa abiria na tukaelekea Dar es Salaam hali ikiwa hivyohivyo na ukiangalia Arusha hoteli zimejaa watalii inatia moyo," amesema Grandcourt.


Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii,  Chana amesema kuwa wafanyabiashara za utalii pamoja na wadau wengine wa sekta hiyo watapata fursa ya kutangaza biashara zao kupitia matukio yatakayoambatana na mkutano huo.

Amesema kuwa mkutano huo utahusisha matukio mbalimbali ikiwemo mkutano wa mawaziri kutoka nchi wanachama, jukwaa la uwekezaji kwa ajili ya kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini.

Waziri Chana asema kuwa pia kutakuwa na mafunzo ya wadau wa sekta ya utalii kwa lengo la kuwajengea uwezo wadau wa utalii kuhusu utangazaji utalii.


Kauli mbiu ya mkutano huo ni 'kujenga upya ustahimilivu wa utalii barani Afrika kwa maendeleo ya kiuchumi ya kijamii'








0 Comments:

Post a Comment