MAJALIWA MKURUGENZI JIJI LA DAR KWA UBADHIRIFU WA BILION Q0



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar Es Salaam, Jumanne Shauri pamoja na watumishi wengine tisa wa jiji hilo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu  wa fedha za Serikali ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 10 zilizokusanywa na hazikuwasilishwa benki kama sheria inavyoelekeza.


 


Agizo hilo linatokana na matokeo ya ukaguzi maalum kuhusu Mapato ya Ndani katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa mwaka wa fedha 2019/2020 hadi 2020/2021 uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). 

Watumishi hao pia wamekabidhiwa kwa Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Dar Es Salaam kwa mahojiano juu ya tuhuma zinazowakabili.


 



Majaliwa ametoa taarifa hiyo leo (Jumatatu, Julai 11, 2022) wakati akizungumza na  viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam, Wabunge, Madiwani pamoja na watumishi wa wilaya ya Ilala katika ukumbi wa Karimjee akiwa katika ziara yake ya kikazi Dar Es Salaam.




Amesema mbali na Mkurugenzi huyo watumishi wengine ni wa jiji waliosimamishwa kupisha uchunguzi ni  pamoja na Tulusubya Kamalamo (Mweka Hazina), James Bangu (Mhasibu Mapato), Abdallah Mlwale (Mtunza Fedha Mkuu) na Mohammed Khais (Mhasibu wa Masoko).


 Majaliwa  watumishi hao wanatuhumiwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo na hivyo kuisababishia Halmashauri hasara ya jumla ya kiasi cha shilingi 10,137,577,401 zilizokusanywa na mawakala na watumishi wa Halmashauri hiyo lakini hazikuingizwa benki.


 


Ametaja watumishi wengine wanaopaswa kuchukuliwa hatua kuwa ni Jesca Lugonzigwa (Afisa Hesabu), Josephine Sandewa (Afisa Hesabu), Tatu Mkangwa (Kibarua) na Felician Maro (Mhasibu Msaidizi) ambao wameisababishia halmashauri hasara ya shilingi 1,214,907,637.


 


Waziri Mkuu ametaja mawakala wanaodaiwa kufanya udanganyifu wa makusanyo ya mapato kwa kuchezea tarehe za PoS  kwa kuzirudisha nyuma na hivyo makusanyo ya kiasi cha shilingi 131,356,400 kutoonekana kwenye taarifa za makusanyo. Mawakala hao ni Pick Trading Ltd na Workers General Supply.


 


“Ripoti ya CAG imebaini kuwa wataalamu wa Halmashauri waliohusika na upotevu wa mapato walikuwa wakiingilia moja kwa moja kati ya mfumo wa LGRCIS na benki na kuandika kwenye mfumo malipo ambayo hayakufika benki kwa lengo la kuficha ukweli wa kasoro na matumizi ya fedha kinyume cha sheria za fedha za umma. Pia wahasibu waliingiza kwenye mfumo kiasi ambacho hakikupelekwa benki kwa lengo la kupotosha taarifa halisi za makusanyo.”

0 Comments:

Post a Comment