KAMISHANA Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Jerald Kusaya amesema kuanzia sasa mashamba yatakayokutwa na mimea ya bangi na mirungi yatataifishwa.
Aliyasema hayo jana wakati akiongea na waandishi wa habari jijini Arusha juu ya operesheni waliyoifanya wilaya za Arumeru na Monduli ambapo walifanikiwa kuteketeza ekari zaidi ya 21 ya mashamba ya dawa za kulevya aina ya bangi.
Kusaya alisema katazo la ulimaji wa madawa ya kulevya limekuwa likitolewa miaka mingi lakini watu wameendelea na kilimo hicho hivyo ni vema sasa wakaanza kutekeleza sheria inayoelekeza maeneo yanayotumiks kulima mimea hiyo yataifishwe.
"Wakati mwingine haya matukio yamekuwa yakirudia mara kwa mara, tumekuwa tukipigana vita madawa ya kulevya lakini watu wengine sijui wana vichwa vigumu namna gani kwani unakuta bado wanaendelea," alisema Kusaya na kuongeza
...Kwasababu sheria inaruhusu katika suala zima la kutaifisha mali na vitu vingine vyote ambavyo ni zao la dawa za kulevya. Kwa hiyo ni vema sasa hili tulitizame kwa mtizamo wa hali ya juu,"
" Kwamba yale mashamba yote ambayo tunayakuta yanalima bangi ama mazao mengine yoyote pamoja na mirungi ni vema sasa, nafikiri ni wakati muafaka yakataifishwa na serikali ili sasa tuweze kukomesha hii biashara,"
"Kwa sababu kama mtu amekamatwa mara ya kwanza au unamuona anarudi akuendelea kufanya biashara ya kilima bangi au mirungi katika hilo shamba ina maana yeye anakaidi na anataka kupingana na serikali,".
"Kwa hiyo la msingi ni hilo kwa hiyo yale mashamba yote ambayo tunakuta yanalima bangi na mirungi ni wakati muafaka sasa kuanza kuyataifisha na kuwa mali ya serikali ambapo wananchi sasa kwa maeneo hayo watakuwa wanapewa maeneo hayo,".
"Kwa maana ya serikali za vijiji ili maeneo hayo yatumiwe kwa matumizi ya umma, yatakuwa mashamba ya umma hivyo wananchi watapanga matumizi bora ya maeneo hayo,".
Aidha Kusaya alisema kuanzia Mei 20 hadi 23 mwaka huu DCEA kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama walifanya oparesheni katika maeneo mbalimbali mkoani Arusha na kufanikiwa kuteketeza hekari zaidi ya 21 ya mashamba ya dawa za kulevya.
Alisema katika oparesheni hiyo walikamata pia bangi kilo 220 katika eneo la Usariver Wilaya ya Arumeru na Wilaya ya Monduli.
"Katika tukio hilo pia watu wanne wanashikiliwa kwa tuhuma za kuzalisha na kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi," alisema kamishina huyo wa DCEA
Alisema wilaya hizo zinakiwango kikubwa cha ulimaji wa bangi na mirungi hivyo aliwataka wanaojihusisha kuacha mara moja ulimaji wa mazao hayo huku akiwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na uzalishaji na usambazaji dawa hizo ili kufikia Tanzania yenye kizazi kisichotumia wala kujihusisha na biashara hiyo.

0 Comments:
Post a Comment