WAKATAA DHAMANA WAENDA MAHABUSU MFALME ZUMARIDI


 Diana Bundala maarufu kama ‘Mfalme Zumaridi' na wenzake 92 wamefunguliwa kesi tatu tofauti na kusomewa mashitaka matatu ya usafirishaji haramu wa binadamu, shambulio la kudhuru mwili na kuzuia maofisa wa Serikali kutimiza wajibu wao.


Wamesomewa mashitaka hayo leo Machi 3, 2022 mbele ya mahakimu tofauti wa mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza.


Mfalme Zumaridi peke yake, amedaiwa kusafirisha binadamu wakiwemo watoto wenye umri chini ya miaka 18 kinyume cha kifungu namba 4(1) (A) na 6(2) (A) cha sheria ya kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu namba 6 ya mwaka 2008.


Katika kesi namba 11/2022, Luvinga amesema Mfalme Zumaridi na wenzake wanane wanadaiwa kufanya shambulio la kudhuru mwili askari wa Jeshi la Polisi waliofika nyumbani kwake kutekeleza wajibu wao kinyume cha kifungu namba 241 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.


Washtakiwa hao pia wanadaiwa kuwazuia maofisa wa Serikali kutimiza wajibu wao kinyume cha kifungu namba 114(A) kifungu kidogo B cha Kanuni ya Adhabu.


Katika kesi namba 12/2022, mwendesha mashataka huyo ameiambia Mahakama mbele ya Hakimu Mfawidhi Mwandamizi Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, Monica Ndyekubora kuwa Zumaridi na wenzake 92 wanadaiwa kufanya kusanyiko lisilo halali kinyume cha kifungu cha 74(1) na 75 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.


Washatkiwa walikana mashtaka hayo katika shauri namba 11/2022 na 12/2022 huku upande wa Jamhuri ukiieleza Mahakama kuwa upelelezi kuhusu mashauri hayo mawili umekamilika na kuomba kupagiwa siku ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali.


Kuhusu shauri namba 10/2022 la usafirishaji haramu wa binadamu linalomkabili Mfalme Zumaridi, mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na uwezo kisheria kusikiliza kesi hiyo.


Licha ya mashtaka namba 11/2022 na 12/2022 kuwa na dhamana huku baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki wakiwa wamejitokeza kuwadhamini, washtaki wote  walikataa dhamana wakisisitiza kuwa wako tayari kwenda mahabusu kuungana na kiongozi wao anayekabiliwa na kesi ya usafirishaji haramu wa binadamu isiyo na dhamana.


Kutokana na uamuzi huo, Hakimu Ndyekubora ameamuru washtakiwa wote kupelekwa mahabusu mpaka  Machi 17,2022  shauri hilo litakaporeja mahakamani hapo kwa ajili ya washatakiwa kusomewa maelezo ya awali.


0 Comments:

Post a Comment