MGOGORO wa
Ngorongoro umechukua sura mpya baada ya Mashirika 20 ya kutetea wafugaji wa asili kutoa tamko wakilaani
udhalilishwaji unaofanywa na watu wenye nia mbaya wakiwemo wanasiasa na baadhi
vyombo vya habari dhidi ya wakazi wa eneo hilo.
Aidha
wamelaani jaribio lolote la kukiuka haki za binadamu katika sakata hilo huku
wakizitaka pande zote zinazohusika na mgogoro huo zijielekeze kwenye kujibu
hoja na sio kushambuliana kwa maneno makali.
Wameyasema
hayo leo Machi 18,2022 kwenye mkutano na
waandishi wa habari uliofanyika jijini Arusha ambapo tamko hilo limesomwa na
Mkurugenzi wa mtandao wa wafugaji nchini, Joseph Parsambei, Afisa Mipango wa
MPDO, Amani Sekino na Msaidizi wa kisheria wa EPO Karatu,Agness Marmo kwa niaba
ya wenzao waliokuwa pamoja nao.
Wamesema wanashauri
itumike meza ya majadiliano katika kupata suluhisho la kudumu la mgogoro huo
huku wakitaka kuwe na ushirikishwaji wa mashirika ya kiraia katika mchakato huo
ili nao waweze kutoa ushauri wao kwani nao ni sehemu ya jamii.
“Tumeendelea
kushuhudia matamko mbalimbali na vita ya maneno kati ya baadhi ya watu wakiwemo
wabunge, Waziri wa Maliasili na utalii na viongozi wa jamii. Tunataka kila
upande uheshimu sheria za nchi, haki za binadamu na utawala bora,” amesema
Parsambei akisoma tamko hilo.
Tamko hili
limekuja siku nane baada ya Waziri Mkuu,
Majaliwa Kasim Majaliwa kukutana na viongozi wa kimila jamii ya kimaasai,
Malaigwanak jijini Arusha na kukabidhiwa na mkuu wa mkoa wa Arusha, John
Mongela jumla ya majina ya kaya 86 zenye watu
453 ambao kwa hiari yao wamekubali kuhama kwenye eneo la Hifadhi ya
Ngorongoro.
Taarifa
iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu ilidai kuwa hayo ni matokeo ya vikao vya kiongozi huyo na wadau wa uhifadhi
vilivyofanyika Februari 14 na 17, mwaka huu kwenye tarafa za Loliondo na
Ngorongoro Wilayani Manyara.
Siku mbili
baadaye Majaliwa alienda kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba mpya 103 kwenye
kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoani Tanga ambazo ni maalum kwa ajili ya
wale wanaohama kwa hiari kutoka kwenye eneo la hifadhi ya Ngorongoro.
Alisema kuwa
kwenye hatua hiyo ya kwanza serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.2
ambapo serikali imeshapima viwanja 2,500 na kutenga eneo la ekeri 1,700 kwa
ajili ya kilimo na malisho huku akisisitiza kuwa serikali itahakikisha haki za
binadamu zinazingatiwa katika zoezi hilo.
Akisoma tamko
la asasi hizo, Marmo amesema kuwa eneo
la tarafa ya Ngorongoro lina ukubwa wa kilometa za mraba 8,000 ambapo mgogoro
ni kati ya serikali na wananchi kwa madai ya ongezeko la watu na mifugo.
Tarafa ya Loliondo
ina ukubwa wa kilometa za mraba 4,000 ambapo eneo la mgogoro ni kiliometa za
mraba 1,500 ya ardhi ya vijiji iliyopo tarafa hiyo pamoja na Sale huku mgogoro
ukihusisha Serikali, Wawekezaji na wananchi.
Marmo amesema
kuwa eneo la tarafa za Loliondo na Sale linatumika na wananchi kwa ajili ya
shughuli zao ikiwemo makazi na ufugaji na yamesajiliwa kwa mujibu wa sheria ya
uanzishwaji vijiji ya mwaka 1978 hivyo wapo hapo kilali.
“Eneo hilo
lina kesi mahakamani hivyo uhuru wa mahakama uheshimiwe na upotoshwaji
unaofanywa na watu wenye maslahi mbalimbali dhidi ya jamii ya wafugaji ukome
mara moja,” amesema Marmo bila kuwataja watu hao na kuongeza.
… Tunaomba Serikali na jamii wakae kwenye meza
huru ya majadiliano na wakubaliane namna ya matumizi ya eneo hilo. Sisi asasi
za kiraia tunaendelea kuwa macho na kufuatilia kwa ukaribu sakata hili.
Marmo amesema
kuwa matumizi endelevu ya ardhi ni suluhisho la mgogoro kwenye eneo hilo hivyo
akashauri wadau wote wajikite katika mrengo huo ili maslahi ya wote yaweze kulindwa.
“Serikali
pamoja na wadau wengine wa maendeleo wawezeshe matumizi endelevu ya ardhi ili
kutoa suluhu ya kudumu ya mgogoro huu,” alisisitiza Marmo.
Kwa upande
wake Sekino amesema kuwa eneo la tarafa ya Ngorongoro lina umuhimu wake na
sheria maalum inayosimamia matumizi yake jambo walilodai kuwa endapo sheria
hiyo ikitumiwa vizuri inaweza kuwa nyenzo ya kutatua mgogoro huo bila kuathiri
maslahi ya upande wowote.
“Ngorongoro
ni nyumbani kwa wafugaji na ni eneo la matumizi mseto hili ni muhimu sana lifahamike
na kuheshimiwa. Utatuzi wa mgogoro huu ni meza huru ya mazungumzo kati ya pande
zote mbili,” alisema Sekino.
Asasi za
kiraia zilizosaini tamko hilo ni pamoja na TPCF, Equity Paralegal Organization,
Leshaabingo, Lareto le sheria, Oseremi, Ngorongoro Paralegal Foundation, Sauti
Zetu Paralegals Organizatio, PALSEF na ALAPA.
Nyingine ni
Embuan Development Organization, CILAO, MPDO, Media Aid Indigenous and
Pastoralist Community, (MAIPAC), Tanzania Pastoralist and Hunter-Gathers Organization,
( TAPHGO), Media Defense Initiative, (MDI), Ngorongoro Education Development
Organization, (NEDO), Tanzania Centre for Research and Information on
Pastoralist, (TCRIP), Indigenous Heartland Organization, (IHO), Mimutie Womea
Organization, (MUMETI) na Intergral
Development Initiative in Ngorongoro,(IDINGO).
0 Comments:
Post a Comment