MBUNGE wa Jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi ameendeleza na ziara yake ya kutembelea jimbo hilo kwa kutembelea Kata ya Kibosho Kirima na kukagua miradi ya maendeleo iliyotekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita tokea aingie madarakani.
Miongoni mwa miradi aliyokagua ni pamoja na ujenzi wa madarasa mawili katika Shule ya Sekondari ya Masoka yaliyojengwa kwa fedha za UVIKO 19 kwa thamani ya shilingi milioni arobaini.
Akitoa ripoti ya mradi huo, Mkuu wa Shule Mwalimu Ahmed Litinji alieleza kuwa mradi huo umekamilika kwa asilimia mia moja.
Mwalimu huyo aliwashukuru wananchi na viongozi mbalimbali kwa ushirikiano wao mkubwa katika utekelezaji wa mradi pamoja na viongozi wa Kijiji cha Boro kwa kuhamasisha nguvu kazi kwani ushiriki wao umesaidia kupunguza gharama za ujenzi na muda wa utekelezaji wa mradi.
Mbunge alimpongeza Mkuu wa Shule kwa mafanikio makubwa aliyoyapata katika kukamilisha mradi kwa wakati, na maendeleo ya shule kwa ujumla.
Diwani wa Kata ya Kibosho Kirima Inyasi Stoki Mushi alimshukuru Mbunge kwa kutembelea Shule hiyo na amemshukuru kwa fedha za mfuko wa MAENDELEO wa jimbo (Tsh Milioni Tatu) ambazo zilitumika kuboresha miundombinu ya shule hiyo.
0 Comments:
Post a Comment