HATIMAYE msafara wa watu zaidi ya 150 waliopanda mlima Kilimanjaro kwa ajili ya kuweka bendera ya Taifa kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro kusherekea miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara umefanikiwa kuweka bendera hiyo kwenye kilele cha Kibo.
Bandera hiyo iliwekwa kileleni hicho kinachofunikwa na theluji ambacho ni kirefu kiliko vyote barani Afrika chenye urefu wa mita 5,895 leo, Desemba 9, mwaka huu na kiongozi wa msafara huo, Kanali, Martin Msumari kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania, (JWTZ).
Msafara huo uliojumuisha watu kutoka maeneo mbalimbali nchini ulianza safari Desemba 5,mwaka huu kwenye geti la Marangu majira ya saa saba mchana baada ya Naibu Spika wa Bunge, Akson Tulia kumkabidhi kiongozi wa msafara bendera hiyo ya Taifa .
Safari hiyo iliyoandaliwa na Shirika la Hifadhi za Taifa, (TANAPA) kwa kushirikiana na Kampuni ya Uwakala wa Utalii ya ZARA ilijumuisha watu kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi ikiwemo TANAPA wenyewe, JWTZ, Bodi ya Utalii Nchini, (TTB), Wakala wa Huduma za Misitu nchini,(TFS), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro,(NCAA), Mamlaka ya Usimamizi wa wanyamapori, (TAWA), Benki ya NBC na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi wa kampuni ya ZARA, Zainab Ansel alisema kuwa wakiwa kama moja ya waandaaji wa safari hiyo alisema wametoa jumla ya watu 250 wakiwemo ya wabeba mizigo na wapishi 185 huku waongoza utalii wakiwa ni 65.
Kiongozi wa waongoza watalii wa kampuni ya ZARA, Faustine Chombo yeye ndiye alikuwa mbele akiongoza njia huku wasaidizi wake waliokuwa na vifaa mbalimbali ikiwemo mitungi ya gesi wakiwa wanatembea pembeni ya msafara huo.
Waongoza utalii hao kutoka kampuni hiyo ya ZARA yenye uzoefu wa zaidi ya miaka 30 kwenye shughuli hizo za kupandisha watalii kwenye mlima huo mbali na kueleza vivutio lakini pia walikuwa wakitoa msaada kwa wapanda mlima waliokuwa wanaonyesha kuwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za kiafya na kuwapatia huduma ya kwanza.
ZARA ambayo imetunukiwa tuzo mbalimbali za ubora ndani na nje ya nchi ambapo kwa mwaka jana pekee, 2020 ilipata Tuzo tano tofauti ikiwemo ya kampuni namba moja kwa kuwapandisha watalii wengi kwenye milima hapa nchi ambapo tuzo hizo zilitolewa na TANAPA.
Waongoza utalii hao wa kike na wa kiume walikuwa wakitoa maelezo kwa wapanda mlima juu ya vivutio mbalimbali wanavyoviona kwenye eneo hilo la ukanda wa chini lenye misitu minene na mito ya maji yenye wanyama wadogo na ndege.
Safari hiyo ya kilometa nane iliwachukua wastani wa saa mbili kufika eneo la kupumzika, kupata huduma ya maliwato ambapo walipata fursa ya kula chakula cha mchana walichokuwa wamefungashiwa na kukabidhiwa wakati wakianza safari kwenye lango la Marangu.
Baada ya mlo huo safari ya kuelekea Mandara iliendelea ambapo mazingira yalikuwa ni yaleyale ambapo ilikuwa inasikika milio ya maji yanayoriritka kwenye miti pamoja na maporomoko ya maji (Water falls) kwenye baadhi ya maeneo ambapo msafara uliwasili Mandara kuanzia majira ya saa 11 jioni.
Kila aliyefika kituoni hapo aliandika taarifa zake kwenye kitabu cha mapokezi kisha waongoza utalii waliwasaidia kuwaelekeza kwenye vyumba vya kulala ambavyo vimejengwa kwa mbao huku wengine wakielekezwa kwenye mahema maalum ya mlimani ambapo watu wote walipata chakula cha usiku kwenye bwalo la kulia chakula.
Siku ya pili ambayo ni Desemba 6, mwaka huu wapanda mlima wote walikuwa tayari kuendelea na safari ya kilometa 11 ambayo huchukua wastani wa saa tano ambapo asubuhi Mwenyekiti wa bodi ya TANAPA, Jenerali Mstaafu, George Waitara aliongea na wapanda mlima hao akiwataka kufuata maelekezo ya waongoza utalii ili waweze kufikia lengo la kufikisha bendera ya Taifa kileleni.
Baada ya hapo Mwenyekiti huyo wa bodi ambaye aliwahi kupandisha bendera hiyo mara kadhaa miaka ya nyuma aliwaaga wapandaji kisha akarejea kwenye lango la Marangu ambapo msafara ulianza safari ya kuelekea Horombo ambapo ni mwendo wa Kilometa 11 kwa mwendo wa kawaida inaweza kuchukua kuanzia saa tano ambapo mpaka saa 12;30 jioni tayari wapandaji wote walikuwa wamefika.
Siku inayofuata wapanda mlima hao walitembea umbali wa kilometa tatu kuelekea kwenye miamba ya pundamilia, (zebra crossing rocks) ambapo walijionea mawe hayo yanayovutia kwa muonekano ambapo michoro hiyo inatokana na madini yaliyokwenye miamba hiyo kutiririshwa na maji hivyo kuweka michoro hiyo ya kuvuti.
Hata hivyo muongoza watalii, Chombo aliwaeleza wapanda mlima kuwa siku hiyo ya tatu anawapeleka eneo hilo kwa lengo la kuwafanya miili yao kuzoea hali ya mlima na kuwa tayari kwa safari ya siku ya nne ambayo ni kilimoeta tisa kuelekea eneo la Kibo safari inayoweza kuchukua wastani wa saa 10 ambapo baada ya kutembea kwa saa tano wanakuwa wamefika eneo la kupumzika ambapo walipatiwa mlo wa mchana na kuendelea safari.
Aidha wapanda mlima hao walipofika eneo la Kibo walipumzika mpaka majira ya saa sita usiku walipoanza safari ya kuelekea kilele cha mlima Kilimanjaro wakiwa na bendera Taifa ambapo safari hiyo ya kilometa sita huchukua wastani wa sita na kuendelea.
Wapanda mlima hao waliposhuka kutoka kileleni walirejea kwenye kituo cha Kibo na kupatiwa vinywaji vya moto kisha wakatembea mpaka kituo cha Horombo ambapo walialala ambapo asubuhi walianza safari ya kuteremka mpaka geti la Marangu watakapopokelewa rasmi.
WAPANDA MLIMA WATOA NENO
Kwa upande wake Kamishina Msaidizi Mwandamizi anayeshughulikia mawasiliano kutoka TANAPA, Paschal Shelutete alisema kuwa asilimia 90 ya wapanda mlima hao waliweza kufika kituo cha Horombo.
Alisema kuwa hiyo inatia matumaini kuwa wengi wataweza kufika kileleni wakiwa na afya njema huku akiendelea kuwasisitiza kufuata maelekezo waliyopewa na waongoza utalii.
Naye mwakilishi wa TFS, Bakar Juma Makeha alisema kuwa wako 10 kwenye msafara huo ambapo mbali ya kushiriki maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru lakini wao kama TFS wanaenda kileleni kuadhimisha miaka 10 tokea kuanzishwa kwa taasisi hiyo.
"Sisi tunaende kieleleni kusherekea miaka 60 ya uhuru na miaka 10 ya taasisi yetu (TFS) kufikisha miaka 10 tokea ianzishwe, tunafurahi kuwa sehemu ya kumbukumbu hii muhimu kwa Taifa letu," alisema Makeha.
Kwa Upande wake Afisa habari na Uhusiano wa TTB, Augustina Makoye aliwapongeza wananchi kwa mwitiko mkubwa waliouonyesha kwa kujitokeza kwa wingi kuupanda mlima huo huku akiwahimiza kuendeleza ari hiyo katika kutembelea vivutio vingine vya utalii vilivopo maeneo mbalimbali hapa nchini.
Mpanda mlima kutoka mjini Moshi, Eddes Mushi alisema kuwaalishiriki kupanda mlima kuadhimisha miaka 60 ya uhuru ikiwa ni sehemu ya kushiriki historia muhimu ya Taifa hili ambapo alisema anapanda mlima huo kwa mara ya pili ambapo mwaka 2019 aliupanda kwa mara ya kwanza na kufanikiwa kufika kileni.
0 Comments:
Post a Comment