KESI ya unyang'anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili imeahirishwa kutokana na shahidi kuwa kwenye sala ya Eid al hajj.
Wakili wa Serikali Mkuu Tumaini Kweka, leo (Julai 20, 2021 )ameieleza mahakama ya hakimu mkazi Arusha mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Odira Amworo anayesikiliza shauri hilo la jinai namba 105/2021.
Wakili wa Serikali Mkuu, Kweka ameieleza mahakama kuwa shauri hili limekuja mahakamani hapo kwa ajili ya kuendelea na ushahidi wa shahidi namba mbili, Numan Jasin, (17) lakini kutokana na sababu za kiimani shahidi huyu ni muislam na kutokana na imani yake jana ndiyo amesali Eid.
"Kusali huko kunaandamana na sherehe zao za kiimani hivyo Jamhuri imeshindwa kumleta aje aendelee na ushahidi wake ila amesema kama kesho tungekuwa tayari kuendelea angekuja lakini nikiangalia ratiba ya serikali kesho (leo) ni siku ya kusali Eid," Kweka aliieleza mahakama na kuongeza.
....Mheshimiwa kutokana na mtiririko wa ushahidi na ulipofikia kwa ushahidi wake itakuwa siyo kisheria kuomba mahakama imuahirishe .....
....Ni rai yetu kwamba shauri hili tuliahirishe mpaka alhamisi Julai 22, 2021 kama mahakama itaridhia katika muda wa mapema zaidi kadiri iwezekanavyo,".
Kwa upande wao mawakili wa utetezi hawakuwa na pingamizi na ombi hilo hivyo hakimu Mkazi mwandamizi, Amworo aliahirisha shauri hilo hadi Julai 22, mwaka huu saa 2:30 asubuhi.
Sabaya na washitakiwa wengine Sylvester Nyegu na Daniel Mbura wanatetewa na mawakili sita ambapo kila mshitakiwa anatetewa na mawakili wawili.
Mawakili Mosses Mahuna na Dancan Oola wanaomtetea mshitakiwa wa kwanza, Sabaya, mawakili Edmund Ngemela na Silvester Kahunduka,
Upande wa Jamhuri unaongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Kweka, akisaidiana a Wakili wa serikali Mwandamizi Abdallah Chavula na Wakili wa serikali Baraka Mgaya.
Katika shauri hilo linalovuta hisia za wengi upande wa jamhuri unatarajia kuleta mashahidi 10 ambapo tayari shahidi wa kwanza Mohamed Saad Hajirini, (45) ameshatoa ushahidi wake mahakamani hapo.
Katika kosa la kwanza Sabaya na wenzake wawili wanashitakiwa kwa unyang'anyi wa kutumia silaha ambapo wanadaiwa kuwa mnamo Februari 9, mwaka huu katika mtaa wa Bondeni jijini Arusha kwa pamoja waliiba sh2,769,000 mali ya Mohames Saad.

0 Comments:
Post a Comment