MAJALIWA: TUMIENI URITHI WA UKOMBOZI KUJIKOMBOA KIUCHUMI

 


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka jamii kuutumia urithi wa ukombozi uliopo nchini kujikomboa kiuchumi na kifikra.


Amesema kuwa ni vyema jamii ambazo zinatumia au zina miliki maeneo au miundombinu ya urithi wa ukombozi wa Afrika ikavitunza na kupata ushauri wa kitaalamu wa kuanzisha makumbusho na kuvutia utalii katika eneo hilo ili kujiongezea kipato.



Ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Mei 21, 2021) wakati wa Ufunguzi wa  Kongamano la kutambua na kuenzi mchango anuai wa historia ya Tanzania katika Ukombozi wa bara la Afrika na Kikao Kazi cha Maafisa Utamaduni na Michezo, kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.


“Nimeambiwa yapo maeneo zaidi ya 225 ya urithi wa ukombozi nchini, maeneo hayo ni fursa kwetu iwapo tutayatumia vyema. Urithi huu wa ukombozi ukiondoka umeondoka, haurudi mara ya pili. Hivyo, ni matarajio yangu kuwa mikoa ya Lindi, Ruvuma (Songea), Mtwara na Mbeya itakuwa mikoa ya kwanza kunufaika na zao jipya hili la utalii wa kiukombozi,” amesema Majaliwa.


Aidha, Waziri Mkuu amesisitiza kuwa jukumu la kuhifadhi na kulinda urithi wa ukombozi tulionao ni la kila mmoja ili vizazi vijavyo viweze kujifunza na kuendeleza.


Akizungumzia kuhusu ufundishwaji wa somo la historia, Waziri Mkuu amewaasa washiriki wa kongamano hilo kuhakikisha ndoto za hayati Dkt. John Magufuli ya kuona somo la historia linafundishwa katika ngazi zote za elimu inatimia. 


Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito wa Watanzania kuweka utaratibu wa kufanya ziara za kwenda kujifunza kwenye maeneo ya ukombozi, “ni wakati muhimu wa kutambua maeneo yenye kumbukumbu muhimu yaliyokomboa nchi yetu na bara la Afrika”

0 Comments:

Post a Comment