VIDEO- TUNA IMANI NA UTAWALA WA SAMIA - WAMILIKI WA VIWANDA

 



WAMILIKI wa viwanda jijini Arusha wameonyesha kuwa na matumaini makubwa kwa serikali ya Rais, Samia Suluhu Hassan kuwa itaendelea kuvisaidia viwanda vya ndani ili viendelee kujiendesha kwa ufanisi huku vikitoa ajira zaidi kwa wananchi. 


Wameyasema hayo kwa nyakati tofauti mwishoni mwa wiki wakati wakitoa salamu za pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuapishwa kuwa Rais huku wakimpa pole pamoja na Watanzania wote kwa kifo cha Hayati, Rais, John Magufuli.

Walisema kuwa, wanaamini serikali itaendeleza yale yote mazuri iliyokuwa imeanza kuyatekeleza hasa ikizingatiwa kuwa Rais, Samia alikuwa Makamu wa Rais hivyo anajua kwa undani mipango yote ya serikali waliyokuwa wamepanga kuitekeleza.

 

Mkurugenzi wa kiwanda cha utengenezaji wa vifaa vya umeme, (TANELEC), Zaihr Saleh alisema wao kama wafanyabiashara wakubwa na wadau wa sekta ya umeme nchini wana matumaini makubwa na uongozi wa Rais, Samia pamoja na Makamu wake Dk Philip Mpango.



"Chini ya uongozi wa Rais, Samia tunaamini viwanda vya ndani  tutaendelea kupewa kipaumbele na support kubwa. Tayari juhudi za serikali kusapporty viwanda vya ndani ili kuwa na uchumi wa viwanda umeshatoa mazao yanayoonekana wazi," alisema Zahir na kuongeza.


"Kwa upande wetu, sisi kama wadau tunaahidi kufanya kazi kwa karibu na kwa bidii na kutoa ushirikiano mkubwa kufanikisha sera za serikali yako,".



"Nina hakika kuwa ufahamu wako mkubwa kuhusu mazingira ya biashara ya nchi yetu na changamoto zake, tutakuwa na fursa nyingi za kukabiliana na changamoto zozote zile za pamoja,".


Kiwanda hicho cha Tanelec kinachoendeshwa kwa ubia kati ya serikali na wawekezaji binafsi wanajishughulisha na kutengeneza vifaa kama transifoma, switchgear na vifaa vingine ambapo inasambaza zaidi ya asilimia 90 ya mahitaji yote ya transifoma nchini kupitia miradi mikubwa ya usambazaji umeme.

Kwa upande wake mkurugenzi wa kiwanda cha Nondo cha Bansal Steel Rolling mills, Teggy Bansal mbali ya kutuma salamu za pole na pongezi kwa Rais Samia na Makamu wake, Dk Mipango naye alisema wanaamini serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wamiliki wa viwanda kama ilivyokuwa ikifanya awali.

Alimtakia Rais, Samia pamoja na wasaidizi wake mafanikio mema katika kutekeleza majukumu hayo mapya huku akiahidi kuwa wataendelea kufanya kazi kwa karibu na serikali.


0 Comments:

Post a Comment