TAKUKURU ARUSHA YAOKOA ZAIDI YA MILIONI 10.3 MILIONI, YAKABADHI WALIOKUWA WAMEDHULUMIWA

 

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, (TAKUKURU), mkoani Arusha imeokoa zaidi ya shilingi milioni 10.3 zilizokuwa zimechepushwa zikiwa ni stahiki zao walipokuwa wafanyakazi wa World Vision mkoani Arusha.

Aidha taasisi hiyo kwa kushirikiana na ofisi ya Taifa ya mashitaka wamewafikisha mahakamani wafanyakazi watatu wa mradi wa utalii wa kitamaduni wa ziwa Eyasi, (LECTP) na kuwafungulia mashitaka ya uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya shilingi milioni 11.4.

Hayo yameelezwa leo Aprili 21, 2021 na mkuu wa TAKUKURU mkoani hapa, James Ruge, wakati akiongea na  waandishi wa habari wakati akiwakabidhi fedha hizo zaidi ya milioni 10.3 waliokuwa wafanyakazi wa world vision, Eliau Laizer na Sarah Msuya.
Mkuu wa TAKUKURU mkoani Arusha, James Ruge akimkabidhi fedha, Sarah Msuya. 


"Laizer na Msuya walipata ajali wakiwa kazini mwaka 2009 lakini hawakuwa wamekipwa fedha zao kama ambavyo sheria ya fidia kwa wafanyakazi inavyoelekeza mpaka TAKUKURU mkoa wa Arusha ilivyoingilia kati mnamo mwezi Februari 2021," alisema Ruge.

Mkuu wa TAKUKURU mkoani Arusha, James Ruge akimkabidhi fedha , Eliau Laizer


Akiongea mara baada ya kukabidhiwa fedha hizo, Laizer alisema kuwa alifanya kazi kwenye shirika la world Vision kwa miaka miwili kuanzia 2007 mpaka 2009.

"Mwaka 2009 mimi na mwenzangu Sarah tulipata ajali tukiwa kazini, katika mazingira yale World Vision wakawa hawatuhudumii kabisa lakini baadae kidogo wakatuhudumia kidogo hali ile ilinikagidha tamaa nikaamua kurudi kusoma," anasema Laizer.

Anasema kunzia mwaka 2010 walianza kufuatilia stahiki zao za kuhudumiwa mara baada ya kupata ajali kazini ambapo walikuwa wakifanya mawasiliano na World Vision kwa njia ya barua ambapo walikuwa wakiwapa matumaini nya kuwalipa lakini hawatekelezi ahadi hizo.

Laizer anadai 2020 waliamua kwenda mahakamani ambapo huko waliwaelekeza kwenda TAKUKURU ambao ndiyo wamewawezesha kupata haki yao.



WATUMISHI WA HALAMASHAURI YA KARATU WABURUZWA KORTINI

Alisema kwenye  shauri la uhujumu uchumi namba 02/2021 lililofunguliwa Aprili 20, 2021 kwenye  mahakama ya wilaya ya Karatu washitakiwa ni wafanyakazi wa mradi wa LECTP, ambao n pamoja na  Leons Gully, Leah Shashi na Ntimi Mwakyembe.

Ruge amesema washitakiwa hao walikuwa wanahusika na kukusanya ushuru wa utalii wa kitamaduni katika kata ya Mang'ola, halmashauri ya Karatu.

Amedai kuwa katika kipindi cha kati ya Julai 2017 na Machi 2018 washitakiwa hao wanadaiwa kukusanya ushuru wa zaidi ya shilingi milioni 11.4 lakini hawakuwasilisha fedha hizo kwenye mamlala husika ambayo ni halmashauri ya Karatu.


TAKUKURU YAWABURUZA MAHAKAMANI WATUMISHI WATATU HALMASHAURI YA LONGIDO

Rege ameeleza kuwa TAKUKURU imewafikisha mahakamani watumishi watatu wa hamashauri ya wilaya ya Longido kwa madai ya kutumia nyaraka za uongo ambapo walishindwa kuwasilisha mifuko 180 ya saruji.

Amesema wafanyakazi hao walifikishwa mahakama ya wilaya ya Longido Aprili 20, mwaka huu na kufunguliwa shitaka la jinai namba 49/2021.

Ruge amesema kuwa washitakiwa hao kutoka idara ya manunuzi ya halmashauri hiyo inadaiwa walipaswa kufanya manunuzi ya mifuko ya saruji 2,400 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya cha Engarenaibor.

"Mifuko 180 haikuwasilishwa, hata hivyo katika taarifa yao waliandika uongo wakionyesha wamewasilisha mifuko yote wakati sio kweli," amesema Ruge

0 Comments:

Post a Comment