MAHAKAMA Kuu kanda ya Arusha imemuru kuuzwa kwa awamu mali za hoteli ya kitalii ya Impala ili kulipa madeni ya malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi wa hoteli hiyo na Naura yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 500.

Wafanyakazi wa hoteli za Impala na Naura Sping wakimsikiliza Kaimu Afisa kazi mkoani Arusha, Emmanuel Mweta aliyekuwa akiwaeza uamuzi uliotolewa na mahakama
Aidha imeamuru fedha zitakazobaki mara baada ya wafanyakazi hao kulipwa zikabidhiwe benki ya NBC ambayo inaidai hoteli hiyo zaidi ya shilingi bilioni 1.5
Jaji, Mohamed Gwae ametoa amri hizo, Januari 8, mwaka huu wakati akitoa uamuzi kwenye maombi ya pingamizi yaliyowasilishwa na kampuni ya Impala na benki ya NBC wakipinga kutekelezwa kwa amri ya ukamataji na uuzwaji wa mali za Impala ili kulipa madeni ya mishahara.
Amri hiyo ilitolewa na Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha , Masijala ndogo ya kazi.
"Kwa kuwa hakuna 'secured creditor' mwingine zaidi ya benki ya NBC ambaye hana pingamizi ila anataka alipwe kile kutakachobaki baada ya mali kuuzwa na wafanyakazi kulipwa madai yao," alisema jaji Gwae akitoa uamuzi wake na kuongeza.
...unaposema kiuzwe ila kisiuzwe chini ya kiwango ambacho kimethaminiwa. Msiuze kwa mradi tu unauza.
Nilikuwa najiuliza kwenye hiyo kesi nyingine ambapo kuna Kiwanja namba 16, 17, 18 na 19 vile ni tofauti na vile 20, 21, 22 na 23 sasa kwa nini kwani vile havitoshi mpaka muuze vyote? ...
...Naomba majibu hawa waliofanyia tathmini manake mimi sivijui sisi tunaongelea kwenye makaratasi hatujaviona najua Impala manake nimelala najua Naura na Ngurdoto,".
Mkurugenzi Pelagia alimfafanualia Jaji Gwea kuwa viwanja hivyo ni tofauti ingawa hivyo ambavyo namba zake zimefuatana vimeungana viwanja viwili vina hati moja.
"Kwa nini msiuze hivi 20, 21, 22 na 23 kwanza hivi kama isipopatikana ndipo muuze hivyo vingine. Wanasema usishangilie kifo cha mwenzako manake na wewe utakuja kufa tu hakuna yeyote atakayeenda mbinguni bila kufa," alisema Jaji Gwea wakati akitoa uamuzi wake huo na kuongeza.
...Mimi natoa amri hii viuzwe kwanza viwanja namba 20 mpaka 23 kama hakuna utimilifu wa hiyo tuzo ndiyo mnaenda kwenye mambo mengine,".
Baada ya uamuzi huo Pelagia alisema kwa kuwa mmliki wa Naura na Impala ni mmoja hivyo fedha zitakazopatikana zitalipa madeni ya yote jambo ambalo jaji aliweleza kuwa hayo hayaihusu mahakama kama wanaweza kufanya hivyo wafanye kinachotakiwa wafanyakazi walipwe kabla mali hazijauzwa.
HOJA ZA BENKI YA NBC
Awali akipitia hoja za waleta maombi, Jaji Gwae alisema kuwa Benki ya NBC iliwasilisha hoja tano za pigamizi kupitia wakili, Wilbard Massawe kutoka kampuni ya Mawalla.
Alisema wakili Massawe aliieleza mahakama kuwa hana shida na kuuzwa kwa mali zilizokamatwa ila izingatiwe tu kwamba benki ina maslahi na benki itakuwa tayari kupata kile kitakachokuwa kimebaki baada ya wafanyakazi kulipwa madeni yao.
"Hata hivyo kwenye hoja zao walisisitiza kutambuliwa kuwa wanaidai Impala hivyo walipwe fedha zitakazobaki mara baada ya wafanyakazi kulipwa madeni yao?" alisema Jaji Gwae akisoma hukumu hiyo.
Alisema kuwa Kaimu afisa kazi mkoani Arusha, Emanuel Mweta, alikubaliana na hilo kwa kile alichoeleza kuwa kwa kuwa NBC haipingi wafanyakazi kulipwa malimbikizo ya mishahara yao.
HOJA ZA IMPALA
Jaji Gwae alisema kuwa, Wakili wa Impala, Richard Massawe aliwasilisha maombi ya pingamizi chini ya hati ya kiapo akidai kuwa mali zilizoamriwa kukamatwa zina thamani kubwa kuliko madeni ya mshahara wanayodaiwa.
Alidai mali zilizoamriwa kukamatwa na kuuzwa zina thamani ya zaidi ya shilingi bilioni tano wakati madeni ya malimbikizo ya mishahara ni zaidi ya shilingi milioni 500.
Jaji alitupilia mbali pingamizi la Impala walilokuwa wanadai Kaimu Afisa kazi wa mkoa, Mweta hakuwa sahihi kufungua maombi hayo mahakamani kwani sheria inataka kamishina wa kazi ndiyo ayafungue.
"Nimepitia sheria nimeona afisa kazi anaweza kufungua mashauri hayo kwani anamwakilisha kamishina wa kazi.Ukizingatia mleta maombi namba moja (Impala) na utayari wake wa kuwalipa wafanyakazi nimeona maombi haya hayana msingi," alisema Jaji Gwae na kuongeza.
...Kwa kuwa yule anayedaiwa kuwa kuna suala la 'guarantee' ambapo mkopo ulichukuliwa (NBC Bank) anasema yeye hana pingamizi. Kama wangekuwa wale ndo wanapinga ingetakiwa waangaliwe manake wale ndiyo wana 'secured creditor',".
Jaji Gwae alisema kuwa kwa kuwa NBC anayetaka atambuliwe baada ya kuuzwa hivyo vitu hivyo kwa msingi huo kuna hivyo viwanja ambavyo vimeshafanyiwa tathmini ya juu bilioni 1.8 lakini wao (Impala) wanasema ni bilioni 8 ingawa hakuna tathmini nyingine iliyofanyika.
"Kwa kuzingatia kwamba kutoka Novemba mwaka jana kesi hii iko hapa mahakamani lakini kwa kuzingatia pia wale wanaowakilishwa na mjibu maombi, Afisa kazi, (wafanyakazi) hawajalipwa mshahara mpaka leo, na kwa kuzingatia kwamba mleta maombi habishi kwamba anadaiwa na wafanyakazi naamuru uuzwaji wa mali iliyokamatwa kwa amri ya msajili iuzwe haraka baada ya kutangaza," alisema jaji Gwea akimaliza kutoa uamuzi kwa upande wa hoteli ya Impala.
HOTELI YA NAURA SPRING
Jaji Gwae pia alisoma uamuzi kwenye maombi ya pingamizi ya hoteli ya Naura Spring dhidi ya utekelezwaji wa amri ya Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha , Masijala ndogo ya kazi ya kuuzwa kwa magari matano na viwanja vinne.
"Sitarudia hoja zote za mawakili na afisa kazi manake ni zilezile ila mali zilizokamatwa ni magari matano na yamefanyiwa utathmini Kesi hii inahusu utekelezaji na 83/2020 ndiyo walifungua kwa msajili," alisema Jaji Gwae.
Alisema "hoja ya mawakili wa Impala kuwa wakurugenzi, Kama Rando (Mrema) hakuwa mkurugenzi lakini Pelagia Mrema yupo lakini pia wasimamizi wa mali za marehemu wapo tulitegemea wafanye kiapo kwamba huyu hakuwa mkurugenzi kubatilisha kikao cha Machi 14, 2019 kilichowateua Rando na Janet,".
....Kama wale kina Herode waliokuwa wanaiwakilisha kampuni kwenye kesi kama wasingekuwa wanatambuliwa na mkurugenzi, Pelagia lakini pia kwa wasimamizi wa mirathi wa marehemu, Mrema, Micheli Mrema wangefanya kiapo cha kuwakana vinginevyo wakili utabaki unasema tu ila wao hawajasema chochote," alisema Jaji Gwae.
WAFANYAKAZI WA IMPALA WANENA
![]() |
| Baadhi ya wafanyakazi wa hoteli za Impala na Naura wakiwa kwenye viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Masijala ndogo ya Kazi Arusha |
Kiongozi wa wafanyakazi wa Impala na Naura Jacob Joel alisema wanaishukuru mahakama na serikali kupitia ofisi ya idara ya kazi ambayo ndiyo waliowawakilusha kwenye shauri hilo.
"Tunaishukuru sana mahakama kwa kutupatia haki yetu maana kwa sasa hivi ni takribani miezi 16 tumekuwa tukisota bila kupata mishahara," alisema Jacob.
Alisema wafanyakazi wa Impala wanadai zaidi ya milioni 397 na wafanyakazi wa Naura wanadai zaidi ya shilingi milioni 107 ikiwa ni malimbikizo ya mishahara.
" Tunadai zaidi zaidi ya milioni 500 maana mpaka sasa bado hawajatusimamisha kazi, bado tunatambuliwa kama wafanyakazi kwa sababu bado hawajatupa barua za kutusimamisha kazi," alisisitiza Jacob.

0 Comments:
Post a Comment