KESI ya madai ya malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi na stahiki mbalimbali ya zaidi ya shilingi milioni 31.9 inayoikabili kampuni ya Tan communication inayomiliki kituo cha Radio Five imeahirishwa baada ya kampuni hiyo kukata rufaa mahakama kuu.
Kampuni hiyo imekata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya kazi Kanda ya Arusha iliyoagiza kukamatwa mali zao na kuuzwa ili kulipa deni hilo.
Naibu Msajili wa mahakama hiyo, Ruth Masamu, aliahirisha shauri hilo Februari 19, 2021 baada ya wakili wa Tan Communication, kuieleza mahakama hiyo kuwa mteja wake ameshawasilisha mahakama kuu notisi ya kusudio la kukata rufaa.
Kampuni hiyo inakata rufaa kupinga uamuzi uliotolewa Juni 16, 2020 na jaji wa Mahakama Kuu, Johannes Masara ambaye alisikiliza shauri hilo namba 151/2020 na kuamua wafanyakazi hao walipwe kwani waliachishwa kazi kinyume na utaratibu.
Naibu msajiri wa mahakama hiyo ,Ruth Masamu baada ya kupokea maombi hayo yaliyoambatana na notisi hiyo aliahirisha shauri hilo hadi Machi 16 mwaka huu.
Kesi hiyo ambayo ilifika mahakamani hapo jana kwa ajili ya waleta maombi, ambao ni waliokuwa wafanyakazi saba wa kituo cha Radio Five kinachomilikiwa na kampuni hiyo kuainisha mali za kampuni hiyo zitakazopigwa mnada ili zipatikane fedha za kuwalipa madeni yao.
Wafanyakazi hao ni pamoja na Geofrey Steven, Monica Nangu , Gloria Kaaya ,Godluck Kisanga , Godfrey Thomas, Akidai kilango na Josephat Nyamkinda.
Wafanyakazi hao walifungua kesi hiyo baada kutoridhika na uamuzi uliotolewa na mahakama ya usuluhishi (CMA) iliyompa ushindi mdaiwa.
Akiongea kwa niaba ya wenzake Geofrey Steven alisema kimsingi wamepokea kusudio la rufaa kwa upande wa wadaiwa na wanachosubiri ni tarehe ya kusikiliza kwa rufaa hiyo.

0 Comments:
Post a Comment