Mwanasiasa mkongwe na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Maalim Seif Sheriff Hamad (76), amefariki dunia.
Akihutubia Taifa kwa njia ya televisheni, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Mwinyi, alisema Maalim Seif alifariki dunia akiwa katika Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa kwa takribani wiki mbili.
Maalim Seif amefariki dunia akiwa ametumikia wadhifa wa makamu wa kwanza wa rais wa SMZ kwa chini ya siku 100 - akiwa sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoundwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2020.
Kifo chake kinahitimisha safari ya kisiasa ya mwanasiasa mashuhuri kuliko wote wa Zanzibar na kiongozi ambaye alizibeba siasa za upinzani katika visiwa hivyo katika muda wa miaka 30 iliyopita.
Mwezi uliopita, katika hatua isiyo ya kawaida, chama chake cha ACT Wazalendo kilitoa taarifa kwa vyombo vya habari iliyoeleza kwamba Maalim na baadhi ya wasaidizi wake na watu ndani ya familia yake walipata maambukizi ya ugonjwa wa korona.
Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar. Natoa pole kwa Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Mwinyi, Familia, Wazanzibari, wanachama wa ACT-Wazalendo na Watanzania wote. Mungu amweke mahali pema peponi,Amina
— Dr John Magufuli (@MagufuliJP) February 17, 2021
Mwisho wa Twitter ujumbe, 2

0 Comments:
Post a Comment