JPM AUBADILI JINA MSITU WA CHATO KUWA SILAYO

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo Januari 27, 2021 amezindua Shamba la Miti Silayo (Awali lililoitwa Shamba la Miti Chato) katika eneo la Butonge, wilayani Chato, Mkoa wa Geita.














 Rais Dkt. John Pombe Magufuli alisema, "Sikutegemea kama siku moja tutakuta miti mizuri katika shamba hili, mmefanya kazi nzuri na kwa kazi kubwa iliyofanywa na Wizara husika, Kamishna wa Uhifadhi wa Misitu pamoja na Maaskari wanaoendelea kulinda misitu hii natamka kuanzia leo shamba hili litaitwa 'Silayo Forest',".


Alisema kuwa  misitu ina faida nyingi za kiuchumi, ambapo katika Mwaka wa Fedha 2019/20 sekta hiyo ilichangia asilimia 3.5 ya Pato la Taifa na asilimia 5.9 ya fedha za kigeni huku ikiiingizia Serikali mapato ya takriban shilingi bilioni 130. 

Rais Magufuli alisema kuwa sekta ya misitu  imeajiri wananchi wapatao milioni moja.

"Kuwa na miti ni kutengeneza ajira hivyo, natumia fursa hii kutoa wito kwa wananchi wa maeneo haya kutoa ushirikiano kwa TFS ili kuhakikisha hekta zote 69,000 zinapandwa miti. Nawasihi kuanza kujiandaa na fursa za kiuchumi zitakazoletwa na uanzishwaji wa shamba hili ikiwemo ujenzi wa viwanda," alisema Rais Magufuli na kuongeza.

"Ni lazima tuachane na utaratibu wa sasa wa kuuza magogo nje ya nchi kwani tunapata hasara sana, hili suala la kusafirisha magogo liwekewe nguvu za kutosha kwani sio tu inatukosesha mapato bali inawakosesha wananchi wetu fursa za ajira....


"Ni vyema tuhakikishe misitu yetu inatumika hapa hapa nchini kwa kutengeneza bidhaa zinazotokana na misitu ili nchi iweze kupata fedha zaidi, natoa wito kwa Wizara ya Maliasili, TFS na wadau kuhakikisha inawajengea uwezo vijana wanaojihusisha na shughuli za kutengeneza bidhaa za miti kwa kuhakikisha mnawapatia ujuzi na mitaji...


"Natoa wito kwa Wizara, TFS na Halmashauri kuwatengenezea mazingira mazuri wafanyabiashara wadogowadogo wanaojihusisha na biashara ya miti na mbao kwani kumekuwa na tabia ya kuwasumbua kwa kuwatoza kodi na tozo kubwa na kuwakamata mara kwa mara...

AONYA JUU YA UHARIBIFU WA MITI

"Pia, natoa wito kwa wananchi kuachana na tabia ya kukata na kuchoma miti hovyo pamoja na kuvamia maeneo ya hifadhi. Aidha, nazihamasisha Taasisi mbalimbali na wananchi kujitahidi kupanda miti katika maeneo yao," alisema Rais Magufuli 

KUANZISHA WILAYA MPYA


"Tunategemea kuanzisha wilaya mpya katika maeneo haya, ahadi hiyo iko pale pale kwani Buselesele na Katoro kunahitajika kuwa na wilaya mpya, nina uhakika Wabunge wa maeneo haya pamoja na Halmashauri husika zitajadili vizuri ili pasitokee mabishano" alisema na kuongeza.


ATOA MSIMAMO JUU YA KUKABILIANA NA CORONA

"Sisi Watanzania hatujajifungia, hatutegemei kujifungia na wala sitegemei kutangaza hilo hata siku moja kwa sababu Mungu wetu yupo hai na ataendelea kutulinda, lakini tutaendelea kuchukua tahadhari za kiafya ikiwemo kujifukiza," alisema Rais Magufuli na kuongeza.


"Mtatishwa sana lakini simameni imara, ninajua wapo baadhi ya Watanzania wameondoka nchini wamekimbilia maeneo mengine kufuata chanjo na wamerudi wametuletea Corona ya ajabu ajabu, simameni imara, chanjo hazifai...


....Ni lazima Watanzania tuwe waangalifu kwa mambo ya kuletewa letewa msije mkafikiria mnapendwa sana, Taifa hili ni tajiri kila mmoja analitamani. Natoa rai kwa Wizara ya Afya isiwe inakimbilia chanjo bila yenyewe kujiridhisha, sio kila chanjo ni ya maana kwa taifa letu, tutafanyiwa majaribio yatakayoleta madhara makubwa,".


Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, sekta ya misitu na nyuki imechangia shilingi bilioni 373 katika Pato la Taifa pia, sekta hiyo kwa nchi nzima inachangia shilingi bilioni 5.2 kwa mwaka katika kodi ya ongezeko la thamani.

"Shamba hili la Chato ni shamba lenye mchanganyiko wa misitu ya asili na ya kupandwa hivyo imelifanya kuwa shamba la kipekee Tanzania la aina hilo, litakapopandwa lote tunatarajia litatoa ajira zaidi ya 30,000," alisema Ndumbaro na kuongeza.


*Aliyosema Naibu Waziri, Maliasili na Utalii, Mary Masanja*


#Tunamshukuru Rais Magufuli kwa kutambua uhifadhi, leo tunashuhudia kuzinduliwa kwa shamba la miti la Chato lenye ukubwa wa hekta 69,000 ambalo ni la pili ukiacha shamba la miti la Saohill lililopo mkoani Iringa lenye ukubwa wa hekta 135,000. 


#Mashamba ya miti ni maono mazuri yanayosaidia kujenga uchumi wa nchi kwani kati ya miaka minne au mitano ijayo tutaanza kuvuna miti na kuanzisha ufugaji wa zao la nyuki utakaopelekea uanzishwaji wa viwanda na ukuzaji wa ajira.


*Aliyoyasema Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS),  Prof. Dos Santos Silayo.*


#Tathmini zilizofanyika zilibaini kuwa kuna upungufu wa malighafi itokanayo na mazao ya miti hivyo ikawekwa mikakati ya kuongeza kasi ya upatikanaji wa malighafi ya miti na mazao ya nyuki ili kukuza uchumi wa viwanda nchini.


#Lengo la kuanzisha mradi huo wa upandaji miti ni kuboresha uhifadhi wa ardhi na mazingira ya eneo hili ili kuhakikisha maeneo hayo yanaendelea kupata mvua za kutosha na kupata malighafi endelevu kwani uhitaji wa mazao ya misitu nchini na nchi za jirani ni mkubwa.


#Tulilenga pia kuongeza wigo wa ajira katika eneo hili ambapo jumla ya ajira takribani 800 kwa mwaka zimetolewa kwa wananchi wanaozunguka eneo hili.


#Tunaahidi kuwa TFS itaendelea kuhifadhi misitu yote nchini kwani ina dhamana kubwa katika maendeleo ya Taifa pia tutaendelea kuimarisha mifumo yetu ya ukusanyaji mapato.


#Tunakushkuru Rais Magufuli kwa miongozo yako unayoitoa inayotuwezesha kuboresha mifumo yetu ya mapato ambapo tangu uingie madarakani tumeongeza ukusanyaji wa mapato kutoka wastani wa shilingi bilioni 75 hadi sasa tunakusanya shilingi bilioni 130 kwa mwaka.


0 Comments:

Post a Comment