Joseph Robinette
Biden Junior - JOE BIDEN
.
Mwanasheria, Makamu wa RAIS wa 47 wa Marekani na SENETA wa miaka mingi wa jimbo la Delaware. Kwa miaka 8 alifanya kazi kwa karibu na RAIS OBAMA. Miaka 4 tangu aondoke IKULU; 2020 anarudi tena kama RAIS wa 46 wa taifa hilo kinara kwa Demokrasia
Alizaliwa mwaka 1942 huko Scranton, Pennsylvania na kukulia New Castle County, Delaware ambapo alipata elimu ya awali, msingi na sekondari kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Delaware ambapo alihitimu Shahada ya sanaa katika historia na sayansi ya siasa mwaka 1965.
Biden hakuwa mwanafunzi hodari, alipata daraja "C" katika shahada yake ya kwanza na alihitimu nafasi ya 506 kati ya wanafunzi 688 waliohitimu pamoja. Mwaka 1965 alijiunga na Chuo Kikuu cha Syracuse, New York na mwaka 1968 alihitimu shahada ya sheria.
Mwaka 1966 alifunga ndoa na Neilia Hunter ambao kwa pamoja walipata watoto 3. Baada ya kumaliza Chuo alirudi Delaware na kuwa wakili wa kujitegemea kabla ya kujiunga na siasa kama kansela wa kauti ya New Castle kutoka 1970 - 1972. Mwaka 1972 akiwa na miaka 29 alichaguliwa kuwa seneta wa jimbo la Delaware, na kumfanya kuwa moja ya maseneta wadogo zaidi kwenye Historia ya taifa hilo.
Mwezi mmoja baadae mkewe na mtoto wao mdogo walifariki kwenye ajali ya gari na watoto wengine wawili walijeruhiwa vibaya jambo lilipopelekea Biden kutaka kuacha siasa, ila watu wake wa karibu walimshauri asifanye hivyo.
Mwaka 1973, aliwania tena kiti cha useneta na alishinda, na kuendelea kushinda tena kwa vipindi 6 mpaka mwaka 2009; na kuwa seneta aliyeiongoza Delaware kwa muda mrefu zaidi.
Mwaka 1977, alifunga ndoa na Mwalimu, Dkt. Jilli Jacob ambao kwa pamoja wamebahatika kupata mtoto mmoja wa kike. Kwa miaka zaidi ya 30 kama seneta, sera zake zilikua zikiangazia zaidi mahusiano ya kimataifa, uhalifu na madawa ya kulevya.
Mwaka 1988, Biden alijaribu kugombea urais wa Marekani ila alijiengua baada ya skendo ya kuibia hotuba ya kiongozi mmoja wa Uingereza.
Mwaka 2008, yaani miaka 20 baadae alijaribu tena kuwania nafasi ya uraisi ila hakufanikiwa kupita ndani ya chama chake cha Democratic; kilichomchagua Seneta Barack Obama kupeperusha bendera yao na Obama alimteua Biden kuwa mgombea mwenza kwenye uchaguzi ambao walimbwaga Seneta wa muda mrefu Marehemu John McCain.
Mwaka 2012, Rais Obama na Makamu wake Biden walishinda tena kipindi chao cha pili na cha mwisho kilichofikia tamati mwaka 2016 na kukabidhi kijiti kwa Rais Donald Trump.
Mwaka 2016 alitazamiwa kugombea Urais ila alikataa kutokana na maombolezo ya kifo cha kijana wake mkubwa Beau aliyefariki mwaka 2015. Alimuunga mkono mgombea wa Democratic, Hilary Clinton ambaye alishindwa vibaya kwenye uchaguzi huo
Aprili 2019, Biden alitangaza nia yake ya kuwania Urais kwa mara nyingine na alijitosa kwenye kinyanganyiro cha ndani ya chama chake cha Democratic ambapo alipokea upinzani mkubwa kutoka kwa Seneta machachari - Bernie Sanders ila baadae aliibuka kidedea na kuchaguliwa kupeperusha bendera ya Democratic akiwa pamoja na mgombea mwenza wake Mwanamama Kamala Harris dhidi ya Rais aliyeko madarakani Donald Trump.
Jana Novemba 7,2020, Joe Biden ameshinda na atakuwa mwanadamu wa 46 kuliongoza taifa hilo.
Makala hii kwa hisani ya @tweetsrifle





0 Comments:
Post a Comment