KESI ya kujaribu kuua inayomkabilia , Ombeni Mollel, (33) imeahirishwa baada ya upande wa jamhuri kuieleza mahakama kuwa upelelezi haujakamilika.
Shauri hilo la jinai namba 19/2020 liliahirishwa leo na hakimu mkazi, Chrisant Chitanda wa mahakama ya wilaya ya Arumeru anayesikikiza shauri hilo.
Wakili wa serikali, Rose Sule alieleza mahakamani hapo kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika hivyo akaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Chitanda aliahirisha shauri hilo mpaka Novemba 18, mwaka huu litakaporudi mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa ambapo mshitakiwa huyo amerejeshwa mahabusu kwenye gereza la mkoa la Kisongo kutokana na mashitaka yanayomkabili kutokuwa na dhamana.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mnamo septemba 25, mwaka huu Mollel anadaiwa alijaribu kusababisha kifo cha mke wake, Veronica Kidemi.
Anadaiwa kufanya tukio hilo maeneo ya Siwandeti wilayani Arumeru Mkoani Arusha.
MOLLEL ATISHIA WAANDISHI WA HABARI
Mshitakiwa huyo Mollel alitishia mwandishi wa habari aliyekuwa akimpiga picha wakati ametoka kwenye chumba cha mahakama baada ya shauri hilo kuahirishwa.
Hali hiyo iliwalazimu askari magereza waliokuwa wakimlinda kumwambia achuchumae huku wakimuhoji sababu za kutishia waandishi.
"Wewe unataka kufanya nini, kwa nini unataka kupiga mwandishi, unataka kuleta matatizo mengine," mmoja wa askari magereza ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja alisikika akimuuliza Mollel.
Hata hivyo mshitakiwa huyo hakujibu chochote hivyo askati magereza hao wakamuingiza kwenye mahabusu iliyopo mahakamani hapo walikohifadhiwa mahabusu wengine.

0 Comments:
Post a Comment