HIZI HAPA SABABU ZA MAWAKALA 522 KUTOAPISHWA ARUSHA MJINI

 

Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Arusha Mjini, Dk John Pima akiwaelekeza mawakala namna ya kujaza fomu za kiapo.


MAWAKALA 522 kutoka vyama mbalimbali vya siasa kwenye jimbo la Arusha mjini hawajaapishwa baada ya kushindwa kutimiza vigezo 


Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Arusha Mjini, Dk John Pima amewaeleza waandishi wa habari leo kuwa fomu za mawakala hao zilikuwa na mapungufu hivyo wakakosa sifa za kuteuliwa na kuapishwa 
Mgombea Ubunge jimbo la Arusha Mjini, kwa tiketi ya CCM Mrisho Gambo akiapishwa pamoja na mawakala wake 




Hata hivyo mawakala hao wamepewa nafasi ya kwenda kufanyia marekebisho mapungufu hayo na warejeshe fomu zao kabla ya muda wa kukamisha zoezi hilo ambao ni leo saa 12 jioni.

Dk Pima alisema kuwa ofisi yake imepokea majina ya  mawakala 11,833 kutoka vyama 15 vya siasa kwa ajili ya kusimamia upigaji kura kwenye vituo vyote 910 vya jimbo la Arusha Mjini.

"Baada ya mapitio kuangalia kama wamekidhi vigezo tumejiridhisha na tumeapisha jumla ya mawakala 11,311 kati ya mawakala 11,833 baada ya kuonekana baadhi ya fomu kuwa na mapungufu," anasema Dk Pima.


Anayataja mapungufu hayo kuwa ni pamoja baadhi ya vyama kuwasilisha majina ya mawakala bila majina ya vituo vya kwenda kusimamia kupiga kura huju barua nyingi zikiwa hazijasainiwa na makatibu wa vyama husika.



"Lakini pia kuna nakala za vitambulisho vilivyotumika hazionekani, ni nakala lakini huwezi kusoma chochote. Baadhi ya makatibu wa vyama wametumia zaidi ya muhuri mmoja kwenye fomu za mawakala wao,"alisema Dk Pima na kuongeza.


"Katibu wa Chama anatumia mihuri zaidi ya miwili kwenye fomu zake zote.Kuna baadhi ya mawakala wametambulishwa na watu ambao kwa mujibu wa sheria hawapaswi kuwatambulisha,"

"Hata hivyo tumevielekeza vyama vyote hivyo kufanyia marekebisho hayo kabla ya muda wa kuapisha kupita ambao ni saa 12 leo (jana) jioni. Wawe wamefanya marekebisho hayo na kama watakidhi vigezo basi tutawaapisha,".

Vyama vilivyowasilisha majina ya mawakala ni pamoja na Chama cha Wananchi, (CUF), Chana Cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), CCK, Chama Cha Mapinduzi, (CCM), ACT Wazalendo, na United Democrat Part, (UDP).

Vingine ni  Demokrasia Makini, ADA TADEA, Sauti ya Umma, (SAU), UMD, NRA, AAMP, ADC, UPDP na NCCR.


0 Comments:

Post a Comment