SABABU ZA OFISA ITIFAKI ANAYEDAIWA KUMNYANYASA MWANDISHI KUNYIMWA DHAMANA




OFISA itifaki (protocol officer) wa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Arusha,  Swalehe Mwidadi, (32), na mfanyakazi wa masijala wa ofisi hiyo ,Amina Mshana, (29) wameburuzwa mahakamani, wakidaiwa kufanya unyang'anyi wa kutumia silaha na kufanya matendo ya ukatili na udhalilishaji wa kumvua nguo na kumpiga picha mwandishi wa habari, Lucas Myovela.

 Wakili wa Serikali, Sabina Silayo  aliwasomea mashitaka hayo  kwenye shauri hilo la jinai namba 153/2018 mbele ya hakimu Mkazi, Patricia Kisinda wa mahakama ya wilaya ya Arusha.

Wakili wa serikali, Silayo alidai mahakamani hapo kuwa washitakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa  kutenda makosa hayo Mei 15, mwaka huu maeneo ya Sakina ambapo walimtishia Myovela kwa panga na kamba ya plastiki kisha kumnyang'anya simu zake mbili, Tecno C7 yenye thamani ya shilingi laki 3 na Samsung yenye thamani ya shilingi elfu 50.

Aliendelea kuieleza  mahakamani hiyo kuwa washitakiwa hao alichukua fedha taslim shilingi elfu 75 na kiasi kingine shilingi 9,500 ambazo zilikuwa kwenye akaunti ya m pesa kisha kuchukua kadi ya benki ya CRDB (ATM Card).

Wakili Silayo alidai katika shitaka la pili washitakiwa hao wote kwa pamoja walifanya matendo ya udhalilishaji kwa kumvua nguo na kumchukua picha za uchi Myovela.

Washitakiwa walikana mashitaka hayo wamepelekwa mahabusu gereza la Kisongo mpaka Juni 6, mwaka shauri hilo litakaporudi mahakamani hapo kwa ajili kutajwa.

Kwa kosa la unyang’anyi endapo wakikutwa na hatia adhabu yake ni kifungo cha mpaka miaka 20 jela.

Umati  mkubwa wa waandishi wa habari ulifurika mahakamani hapo kufuatilia shauri hilo.


0 Comments:

Post a Comment